Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni miaka 40 sasa tangu tumetokomeza ndui:WHO

 Chanjo dhidi ya ndui kwa watu wote katika eneo la Inchon na Seoul nchini Korea
UN Photo/Grant McLean
Chanjo dhidi ya ndui kwa watu wote katika eneo la Inchon na Seoul nchini Korea

Ni miaka 40 sasa tangu tumetokomeza ndui:WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO leo limeadhimisha miaka 40 tangu kutokomeza ugonjwa wa ndui duniani likisema ni mafanikio makubwa ya kihistoria ambayo yanadhihirisha haja ya haraka ya kuwekeza katika usalama wa afya ya kimataifa na huduma za afya kwa wote.

WHO inasema maadhimisho ya leo ni kukumbuka wakati wa kihistoria 9 Desema 1979 ambapo ilitangazwa rasmi ndui imetokomezwa baada ya kuthibitishwa na kamati ya kimataifa kwa ajili ya utokomezaji wa ndui na miezi mitano baadaye Mei 1980 kikao cha 33 ya baraza la afya duniani kikatoa azimio rasmi la kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

Shirika hilo linasema ndui ulikuwa ugonjwa mbaya sana ambao ulisababisha mateso na vifo katika karne iliyopita ambapo takwimu zinaonyesha watu milioni 300 walikufa nan dui katika karne ya 20 pekee.

Pia ugonjwa huo uliwaacha wengi na matatizo ya ngozi, maumivu makali, ulemavu na theluthi moja ya watu wote waliopata ndui walikufa. Ugonjwa huo ulisambaa kote duniani na kudumu kwa karne. Kisa cha mwisho cha nduo kwa mujibu wa WHO kiliripotiwa Somalia 1977.

Baada ya kuripotiwa kwenye mkutano wa Baraza la afya duniani mwaka 1948 na mwaka 1958 kwenye muungano wa Soviet , WHO ilizindua mkakati kabambe wa kutokomeza nduo mwaka 1967. Na leo hii ndui ndio ugonjwa pekee uliowahi kutokomezwa ukiwa ni dhihirisho la wazi wa nini tunaweza kufikia endapo nchi zote zinashirikiana na kufanya kazi pamoja limesema shirika la afya.

WHO inasema mafanikio hayo yakutokomeza ndui yaliipa dunia ari ya kuzindua program za chanjo kwa watoto na baadaye mkakati wa kutokomeza polio.

Na yale ambayo dunia imejifunza katika kutokomeza ndui yamechangia katika kuimarisha hatua za kufuatilia magonjwa ambazo zimefanikisha katika juhudi za leo za kutokomeza polio.