Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuchangia CERF ni uwekezaji bora zaidi- Guterres

Wanawake wakiteka maji katika mradi wa maji uliofadhiliwa na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Dolow nchini Somalia. IOM, WFP na mashirika mengine waliweze kusaidia mahitaij ya wakimbizi hao kutokana na mfu
WFP/Georgina Goodwin
Wanawake wakiteka maji katika mradi wa maji uliofadhiliwa na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Dolow nchini Somalia. IOM, WFP na mashirika mengine waliweze kusaidia mahitaij ya wakimbizi hao kutokana na mfuko wa CERF.

Kuchangia CERF ni uwekezaji bora zaidi- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Kuwekeza katika mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF si tu kunafanikisha usaidizi wa kibinadamu bali pia ni kuwekeza katika kuboresha kazi za chombo hicho chenye wanachama 193, amesema Katibu Mkuu Antonio Guterres jijini New  York, Marekani hii leo wakati akifungua kikao cha ngazi ya juu cha kuchangia mfuko huo  ulioanzishwa mwaka 2006.

CERF tangu kuanzishwa kwake imeshaelekeza zaidi ya dola bilioni 6 za usaidizi kwa mataifa 104 yaliyokumbwa na zahma, fedha hizo zikitolewa kwa kasi kubwa na hivyo kuwa jawabu la wale walio na uhitaji.

Guterres amesema ni dhahiri shairi kuwa mfuko huo umekuwa wa msaada mkubwa wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa umekabiliwa na ukata akitoa ushuhuda wa jinsi CERF imekuwa jawabu kwa waliokumbwa na majanga kama vile vimbunga, mafuriko na vita.

CERF ni mkombozi kwa wenye  uhitaji

“Saa chache tu baada ya kimbunga Idai kupiga maeneo ya kusini mwa Afrika, CERF ilielekeza dola milioni 20 kusaidia wadau wa kibinadamu nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe na misaada ilifikia mamia ya maelfu ya watu waliokuwa na mahitaji  ya dharura ya maji, huduma za afya na nyinginezo,”  amesema Katibu Mkuu.

Kimbunga Idai kilifuatiwa na kimbunga  Kenneth ambacho kilipiga visiwa vya Comoro na Msumbiji ambapo tena “CERF ilielekeza dola milioni 12 kusaidia watu wapate maji safi na huduma za kujisafi, makazi, chakula na huduma ya afya,”  amesema Katibu Mkuu.

UN News Kiswahili

Ameongeza kuwa fedha kutoka CERF zimesaidia kuepusha njaa katika eneo la pembe ya Afrika baada ya mapigano na ukame uliopitiliza kusababisha viwango vya juu vya njaa ilhali huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, CERF nayo imeokoa manusura wa Ebola.

Ni kwa kuzingatia kuwa majanga yanaendelea kunyemelea dunia kila uchao, Katibu Mkuu amesihi nchi wanachama wa  Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wasaidie kutunisha mfuko wa CERF akitoa shukrani kwa ukarimu wan chi 127 na wahisani waliochangia akisema kuwa, “tunakaribisha mchango wa kiwango chochote kile. Hii leo CERF inakabiliwa na uhitaji mkubwa zaidi tangu ianzishwe.”

Mahitaji kuendelea kuongezeka kila uchao

Guterres amenukuu tathmini ya hali ya usaidizi wa kibinadamu iliyotolewa hivi karibuni ikisema kuwa mwaka 2020 watu milionii 168 watahitaji misaada ya kibinadamu, ikiwa ni idadi iliyovunja rekodi na fedha inayohitajika ikiwa n idola bilioni 28.8.

Hata hivyo amesema ni nadra sana shida zinazokumba wananchi kupatiwa kipaumbele kwenye vyombo vya habari, vivyo hivyo katika kuvutia watoa misaada.

Ni kwa mantiki hiyo miaka mitatu iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutaka kuongezwa kwa lengo la upatiaji fedha CERF kutoka milioni 450 kwa mwaka hadi dola bilioni 1 ambapo Katibu Mkuu amesema, “chonde chonde ungeni mkono ahadi ya Baraza Kuu la kuongeza kiwango hadi dola bilioni 1 kwa mwaka. Umoja wa Mataifa unahitaji CERF thabiti na yenye kuchukua hatua haraka. Hebu na tuweke jitihada zetu na rasilimali zetu na kuokoa maisha zaidi.”

Miradi ya dharura ilenge  makundi yote hususan ya watu wenye ulemavu, wanawake, wasichana na watoto- Lowcock

Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura ya kibinadamu, OCHA.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Bwana Lowcock amesema kuwa, mahitaji yasiyokuwa ya kawaida ya kibinadamu kwa mwaka huu yalihitaji hatua za dharura kwa watu mamilioniya watu waliokumbwana zahma katika mataifa 46.

Tweet URL

Hata hivyo amesema kuwa changamoto kubwa zinatarajiwa na kwamba mwelekeo wa mwaka ujao umegubikwa na kiza.

 “Mtu mmoja kati ya watu 45 duniani kote anatarajiwa kuhitaji msaada wetu. Hii ni idadi kubwa zaidi ambayo itahitaji takribani dola bilioni 29,” amesema Bwana Lowcock.

Kwa kuzingatia hilo, ametaja mambo mawili ya kusaidia CERF kusonga mbele katika usaidizi ambapo mosi ni kuwa mbele zaidi kabla ya janga kutokea na cha kutumiwa ni takwimu zinazoonyesha dhahiri kuwa janga halikwepeki. Pili amesema ni kujumuisha watu wote na kuona miradi yote inalenga wale wenye uhitaji zaidi.

“Nasihi wawakilishi wakazi na waratibu wa masuala ya kibinadamu katika nchi wazingatia masuala ya ukatili wa kijinsia na elimu katika majanga yaliyodumu muda mrefu,” amesema mkuu huyo wa OCHA akimaanisha kuwa miradi yoyote ya usaidizi izingatia mahitaji ya  makundi yote ikiwemo watu wenye ulemavu.