Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP katika harakati za kuwafikia watu 700,000 na msaada wa chakula nchini Haiti

Shule zimefunguliwa nchini Haiti na pichani watoto katika shule ya Kenscoff wananufaika na mgao wa chakula shuleni unaowezeshwa na WFP, Haiti na Canada.
WFP/Alexis Masciarelli

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango  wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limeanzisha operesheni nchini Haiti ya kufikisha msaada wa dharura wa chakula kwa watu 700,000 kwa kipindi cha miezi minane ijayo. Brenda Mbaitsa na ripoti kamili.

WFP inasema kuwa bila ya msaada nchini Haiti,  hali inaratajiwa kuwa mbaya ziaidi na kwamba ili kuweza kuwafikia watu walio na mahitaji zaidi ya chakula WFP imetoa ombi la dharura la la dola milioni 62.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi, Bettina Luescher ambaye ni msemaij wa WFP ameeleza kuwa ili kufika sehemu zilizo ngumu kufikika au hatari kwa njia ya barabara, WFP imeanzisha huduma za ndege na kukodisha ndege inayoweza kubeba abiria 22 na tani 4 za mizigo. 

Ndege hiyo imekuwa ikitumika kusafirishia wafanyakazi wa kutoa misaada kutoka mashirika 24 kote nchini.

Wananchi wa Haiti wakiwa wamepanga foleni kupokea msaada wa chakula kutoka WFP kwenye kitongoji cha Chansolme kilichopo wilaya ya Kaskazini-Magharibi mwa Haiti.
WFP/Alexis Masciarelli
Wananchi wa Haiti wakiwa wamepanga foleni kupokea msaada wa chakula kutoka WFP kwenye kitongoji cha Chansolme kilichopo wilaya ya Kaskazini-Magharibi mwa Haiti.

Ameongeza kuwa kwa sasa familia nchini Haiti zinapitia kipindi kigumu ikiwemo kuongezeka kwa bei za bidhaa, kushuka kwa thamani ya fedha na kupungua kwa mazao ya kilimo, mambo ambayo Bi. Luescher amesema yamemuathiri mmoja kati ya raia watatu wa Haiti au jumla ya watu milioni 3.7.

Kati ya hao, watu milioni moja wanakumbwa na njaa kwa mujibu wa ripoti inayohusu usalama wa chakula iliyotolewa mwezi Oktoba mwaka huu.

Halikadhalika, migogoro nayo inazuia usafirishaji wa misaada ya kibinadamu kwenye barabara kuu za kati ya mji mkuu Port-au-Prince na eneo la Artibonite kusini mwa Haiti.

Kwa ujumla msemaji huyo wa WFP amesema katika kipindi cha wiki tatu zilizopita karibu watu 23,000 wamepokea chakula cha dharura eneo la Kaskazini-Mashariki  ambalo linatajwa na serikali kuwa linakumbwa na ukosefu mkubwa zaidi wa chakula nchini humo.