Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko na vimbunga vilitawanya watoto 761,000 Karibea kati ya 2014 na 2018

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 akiwa amesimama mbele ya kifusi cha taka baada  ya kimbunga Irma kupiga pwani ya kaskazini ya jamhuri ya Dominika
© UNICEF
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 akiwa amesimama mbele ya kifusi cha taka baada ya kimbunga Irma kupiga pwani ya kaskazini ya jamhuri ya Dominika

Mafuriko na vimbunga vilitawanya watoto 761,000 Karibea kati ya 2014 na 2018

Msaada wa Kibinadamu

Idadi ya watoto waliotawanywa na mafuriko na vimbunga katika visiwa vya Karibea imeongezeka mara sita zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imesema ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Katika visiwa vya Bahama moja ya maeneo ambayo yalikumbwa na kimbunga Dorian athari zake ziko bayana na miongoni mwa walioathirika zaidi walikuwa ni watoto kama John mwenye umri wa miaka 8 , nyumba yao ilisambaratishwa kabisa na kimbunga hicho eneo la Abaco. John anasema kuwa, “baadhi ya ndugu wa familia yetu wamekufa na marafiki zangu wamehamia kwingine. Sikuwa na vitu vya kuchezea , sichezi tena na wanasesere.”

Huyo ni mfano tu wa maelfu ya watoto walioathirika na kutawanywa kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF iitwayo “watoto waliotawanywa Karibea, jinsi gani vumbunga vitokanavyo na mabadiliko ya tabianchi vinavyotawanya watoto”ambayo imebaini kwamba watoto takribani 761,000 waliwalikuwa wakimbizi wa ndani kwa sababu ya vimbunga vilivyokumba visiwa vya Caribbea kati ya mwaka 2014 hadi 2018.

Tweet URL

Na hilo ni ongezeko la karibu watoto600,000 ikilinganishwa na watoto 175,000 waliotawanywa kati ya mwaka 2009 hadi 2013.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore  amesema ripoti hii ni kumbusho kwamba mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ni mgogoro wa haki za mtoto.

Watoto kutoka katika mataifa yaliyoathirika na vimbunga na mafuriko kote ulimwenguni ni miongoni mwa walio hatarini zaidi kwa maisha yao na haki zao kukiukwa.

Tayari wanahisi athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa hivyo serikali na jamii ya kimataifa zinapaswa kuchukua hatua sasa ili kupunguza athari hizo kuwa mbaya zaidi.

Wengi wa watoto hao mpaka sasa wameishia kwenye makazi ya muda na kutojua hatma ya mustakbali wao. Britney mwenye umri wa miaka 13 alinusurika kifo wakati wa kimbunga Dorian visiwani Bahama na anasema, “tuliogopa sana kusema ukweli, tulidhani tungekufa na tuliporejea tulikokuwa tunaishi tuliona maiti zimetapakaa kila mahali, tuliogopa sana.”

Ripoti inasema sababu kubwa ya watoto wengi kutawanywa ni ongezeko la mfululizo wa vimbunga kati ya mwaka 2016 na 2018 na watoto zaidi ya laki nne walitawanywa katika visiwa vya caribbea mwaka 2017 pekee.

Pia ripoti inaonya kwamba bila hatua madhubuti za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi , ongezeko la vimbunga litasababisha idadi kubwa zaidi ya watoto kutawanywa katika muongo ujao.

Mijengo Dominica zinakarabatiwa baada ya kisiwa hicho kuharibiwa na kimbunga Irma. (Februari 16 2018)
UNDP/Zaimis Olmos
Mijengo Dominica zinakarabatiwa baada ya kisiwa hicho kuharibiwa na kimbunga Irma. (Februari 16 2018)

Na inatoa wito kwa serikali kuchukua hatua kuzisaidia jamii kujiandaa, kuwa na mnepo na kulinda Watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kujumuisha Watoto katika mikakati na mipango ya kudhibi mabadiliko ya tabianchi, kuwalinda kutokana na athari, kuwapa ulinzi watoto waliotawanywa na fursa ya huduma muhimu kama elimu na afya, kuzisaidia familia zilizotawanywa kuishi pamoja na kuhakikisha kwamba watoto waliotawanywa wana haki za kisheria endapo watakimbilia nchi nyingine.