Heko Brazil kwa kuridhia ombi la ukimbizi la wavenezuela- UNHCR

6 Disemba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekaribisha  uamuzi wa Brazil wa kutambua maelfu ya wasaka hifadhi kutoka Venezuela kama wakimbizi, hali inayoashiria kuwa wanaweza kukubaliwa maombi yao ya ukimbizi nchini humo. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Kudorora kwa uchumi na hali ngumu ya maisha nchini Venezuela vimesabiasha wavenezuela milioni 4 wakimbie nchi yao tangu mwaka 2014 na hali imezidi kuwa ngumu na wamesaka hifadhi maeneo mbalimbali ikiwemo Brazil.

Na baada ya muda mrefu wa kusubiri kukubaliwa maombi yao ya ukimbizi Brazil, hatimaye kamati ya kitaifa ya masuala ya wakimbizi nchini Brazil, CONARE, imetangaza uamuzi wa kuridhia ombi hilo ikimaanisha ya kwamba maombi ya wavenezuela wanaosaka hifadhi Brazil yapatiwa mchakato wa haraka bila kuhitaji kuhojiwa, ikimaanisha kuwa wamekidhi vigezo.

Ni kwa mantiki hiyo hii leo huko Geneva, Uswisi, msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema kwamba, “hatua hii ni ya kihistoria katika ulinzi wa wakimbizi katika ukanda huo na inafuatia uamuzi wa mwezi Juni mwaka huu wa CONARE wa kutambua kuwa  hali ya Venezuela inatisha na ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mujibu wa azimio la Cartagena la mwaka 1984 kuhusu wakimbizi.”

Kwa mujibu wa kipengele kipya, wasaka hifadhi wa Venezuela  wanapaswa wawe wanaishi Brazil na wasiwe na kibali kingine chochote cha kuishi nchi nyingine na wawe na umri wa zaidi ya miaka 18 pamoja na nyaraka ya kuthibitisha ni raia wa Venezuela na asiwe rekodi yoyote ya uhalifu nchini Brazil.

Hadi sasa wakimbizi 21,000 wa Venezuela walioko Brazil wamenufaika punde tu baada ya uamuzi kutangazwa ambapo Bwana Baloch amesema, “mamlaka za Brazil zinakadiria kuwa takribani wavenezuela 224,000 hivi sasa wanaishi nchini humo. Na kwamba kila siku takribani wavenezuela 500 wanavuka mpaka kuingia Brazil na wengi wao wanapitia jimbo la kaskazini la Roraima.”

Ameongeza kuwa serikali ya Brazil kwa upande wake inaendelea kuongoza hatua za kibinadamu za kusaidia wakimbizi wa Venezuela walio hatarini zaidi huku ikisongesha harakati bunifu za kuwasaidia kijamii na kiuchumi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud