Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hebu tunusuru nchi 32 zisizo na baharí ili nazo zisiachwe nyuma kimaendeleo- UN

Kasi ya usafirishaji mizigo nayo ni moja ya sababu za kufanya biashara iwe ngumu au rahisi
IMO
Kasi ya usafirishaji mizigo nayo ni moja ya sababu za kufanya biashara iwe ngumu au rahisi

Hebu tunusuru nchi 32 zisizo na baharí ili nazo zisiachwe nyuma kimaendeleo- UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kumefanyika mkutano wa tathmini ya kati na ya kina ya mpango wa utekelezaji wa Vienna kuhusu mataifa yanayoendelea yasiyo na bahari  LLDCs, ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema changamoto zinazokabili mataifa hayo 32 ni dhahiri shairi.

“Mengi yao yako maeneo ya ndani zaidi na hayazungukwa na bahari na njia nyingine za kuyaunganisha na mataifa mengine kama vile barabara, reli, mawasiliano ya kisasa na pia yako nyuma sana kimaendeleo,”  amesema Katibu Mkuu.

Amesema kuwa changamoto hizo kwa pamoja zinaongeza gharama  huku zikipunguza fursa na kuzuia muunganiko wa mataifa hayo katika chumi za kimataifa na kikanda na hivyo, “kuchochea umaskini na kukwamisha maendeleo endelevu.”

Mathalani amesema kiwango cha biashara bado ni kidogo, “mataifa hayo yanachangia asilimia 1 tu ya biashara ya nje duniani. Zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa wanazouza nje ni mazao ya msingi na maliasili. Miundombinu bado haitoshi, uwekezaji wa kigeni ambao mara nyingi ni kichocheo cha ushindani umeendelea kupungua. Na kama ilivyo mataifa mengine, nchi zisizo na baharí nazo zimezidi kukumbwa na janga la mabadiliko  ya tabianchi.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema kupitia mkakati huo wa Vienna uliopitishwa miaka 5 iliyopita, vikwazo hivyo vinaweza kusambaratishwa akitolea juhudi ambazo tayari zimeanza kuchukuliwa kuimarisha muunganiko kwa njia ya barabara na kuendeleza maeneo ya mpito ya biashara na kiuchumi.

“Mkataba wa Muungaon wa Afrika wa eneo huru la biashara barani Afrika, AcFTA na mkataba wa uwezeshaji biashara wa shirika la biashara duniani, WTO, vinatoa fursa kwa nchi zisizo na bahari za kuziunganisha na masoko ya nje na minyororo ya thamani ya kibiashara duniani,amesema Bwana Guterres.

Ametoa wito pia kwa wadau wa maendeleo kushirikiana na kumasisha rasilimali za ndani nan je na kuzielekeza katika maeneo yanayochochea ukuaji na pia yenye vipaumbele vya juu.

Bwana Guterres ametolea mfano maeneo ya sekta binafsi akisema ni lazima kusaidia mataifa hayo kukuza sekta hizo na kuchochea mazingira ya biashara pamoja na usaidizi wa kiufundi na kuzijengea uwezo.

Zaidi ya yote amesema kwa kuwa sera au uamuzi wowote unategemea takwimu, “ni vyema kuimarisha mifumo ya kitaifa ya takwimu ya mataifa hayo.”

Biashara mtandaoni inasaidia bidhaa kama hizi zinazotengenezwa huko huko Manzini, Swaziland kuweza kupatikana hata kwa wahitaji barani Asia
FAO/Giulio Napolitano
Biashara mtandaoni inasaidia bidhaa kama hizi zinazotengenezwa huko huko Manzini, Swaziland kuweza kupatikana hata kwa wahitaji barani Asia

Amewakumbusha washiriki kuwa kwa kuwa azimio wanalopitisha leo linataka kusaidia kubadili nchi zisizo na bahari kuwa nchi zinazounganishwa kwa ardhi kwa ajili ya ustawi na fursa, basi “tuunganishe nguvu zetu kusaidia nchi hizi 32 zinazoendelea zifanikishe mabadiliko endelevu na kuwa na maisha yenye hadhi kwa zaidi ya watu milioni 500 ambao mataifa hayo ni nyumbani kwao.”

Athari za tabianchi kwa nchi zisizo na baharí ni kubwa zaidi pia- Profesa Bande

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Tijjan Muhammad-Bande amesema mpango wa utekelezaji wa Vienna ulilenga kuchangia katika harakati za kutokomeza umaskini kwa nchi hizo zisizo na baharí.

 Ni kwa mantiki hiyo amesema anatambua juhudi za nchi wanachama wa  Umoja wa Mataifa za kupitisha azimio la kisiasa hii leo, akisema ni “ishara ya uthabiti wa ushirikiano wa kimataifa kama chombo cha kuweza kusaidia masuala yanayokabili dunia nzima. Kwa njia hii tumeshughulikia masuala yanayogusa nchi zinazoendelea lakini hazina bahari, nchi za mpito ambako mizigo inapita kuelekea kwenye nchi hizo na pia nchi zilizoendelea.”

Amesema azimio hilo la kisiasa linawezesha kuunganisha mkakati wa Vienna na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema kuwa, hatua hiyo ni sahihi kwa kuwa kwa mwelekeo wa sasa nchi zisizo na bahari zitasalia nyuma kwa kuwa, “ukuaji wao wa uchumi umeporomoka katika miaka 5 iliyopita na theluthi moja ya wananchi wao ni hohehahe.”

Na zaidi ya yote madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni mabaya zaidi, ikiwemo vimbunga, ukame na mafuriko akitolea mfano Malawi na Zimbabwe.

“Miezi 9 iliyopita, Malawi na Zimbabwe ambazo hazina bahari zilipata madhara makubwa kutokana na kimbunga Idai kilichopita maili nyingi kutoka bahari ambayo wao hawaioni,”  amesema Profesa Bande.

Kwa mantiki hiyo amesihi washiriki wawe na mjadala wa dhati juu ya kutekeleza yaliyomo kwenye azimio hilo la kisiasa ili kunusuru mataifa yasiyo na bahari duniani.

Mkakati wa Vienna una vipaumbele vingapi?

Mpango huo wa utekelezaji wa mkakati wa Vienna una vipaumbele vikuu 6. Vipaumbele hivyo ni masuala ya msingi kuhusu maeneo ya mpito, uendelezaji na utunzaji wa miundombinu, biashara ya kimataifa na uwezeshaji, ushirikiano wa na utangamano wa kikanda, marekebisho ya kimuundo ya kiuchumi na mbinu za utekelezaji.