Watoto milioni 2.2 kupata chanjo ya surua Kivu Kaskazini DRC:WHO

5 Disemba 2019

Watoto takribani milioni 2.2 wanatarajiwa kupewa chanjo dhidi ya surua katika awamu ya pili ya kampeni chanjo dhidi ya  ugonjwa huo kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambako juhudi zinaendelea hivi sasa kukabiliana na mlipuko wa pili mkubwa kabisa wa ebola. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la afya ulimwenguni WHO,  nchi ya DRC mbali ya ebola hivi sasa inakabiliwa na mlipuko mkubwa na mbaya zaidi wa surua ukiathiri majimbo yote 26 ya nchi hiyo.

Tangu kuanza kwa mwaka huu 2019 kumekuwa na visa vinavyoshukiwa zaidi ya 250,000 na vifo zaidi ya 5000 vingi ni miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Kampeni hii shirika la afya duniani linasema ni awamu ya pili ya juhudi za kutoa kinga na itafuatiwa na awamu ya tatu  na ya mwisho iliyopangwa kutolewa katika majimbo kumi yaliyosalia ya Bas Uélé, Equateur, Haut Katanga, Haut Lomami, Haut Uélé, Kasai Oriental, Lualaba, Maniema, Mongala na Tshuapa.

Kampeni hiyo itakayofuata hatimaye itakuwa imewafikia watoto milioni 18.9 katika nchi nzima ifikapo mwishoni mwa mwaka hu una ikiwalenga zaidi hususan wale ambao huenda walikosa chanjo za kawaida.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Dr Matshidiso Moeti amesema “wakati mlipuko wa Ebola nchini DRC umepatiwa msukumo mkubwa wa kimataifa na mchakato ukiendelea katika kuokoa maisha , tunapaswa kutosahau dharura na mahitaji mengine ya haraka ya kiafya yanayoikabili nchi hii. Kampeni hii mpya ya chanjo inalenga kuwalinda Watoto Kivu Kaskazini pamoja na maeneo mengine ya nchi kutokana na ugonjwa ambao unaweza kuzuilika kirahisi na chanjo.”

Ameongeza kuwa kiwango kidogo cha watu kupewa chanjo na kiwango kikubwa cha utapiamlo vimechangia kusambaa kwa mlipuko wa surua na idadi kubwa ya vifo.

Amesisitiza kuwa kampeni hiyo ya chanjo Kivu Kaskazini inafanyika kukiwa na changamoto kubwa ya usalama hususan katika maeneo ya Beni na Masisi.

Ameongeza kuwa kuimarisha chanjo ya mara kwa mara , kufuatrilia visa vya surua na kudhibiti visa hivyo kutachangia kukomesha mlipuko wa sasa na kutokomeza surua kama tatizo kubwa la afya ya umma DRC.

WHO inasema ukosefu wa fedha unaathiri juhudi za kampeni ya chanjo.

Hadi leo dola milioni 27.5 zimekusanywa lakini bado dola zingine milioni 4.8 zinahitajika ili kukamilisha awamu zote za kampeni ya chanjo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Watoto 4500 wamepoteza maisha kutokana na surua DRC:UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetaka mkazo utolewe pia kukabiliana na ugonjwa wa surua ambao linasema unaua idadi kubwa ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kuliko hata Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.