Wahitaji miaka 1,000 kupata sentimeta 1 ya tabaka la juu la udongo- FAO

5 Disemba 2019

Hii leo ikiwa ni siku ya udongo duniani, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na kilimo duniani, FAO linataka hatua zaidi kuepusha mmomonyoko wa udongo kwa ajili ya mustakabali bora.

Mkurugenzi wa FAO anayehusika na masuala ya ardhi na kampeni ya siku ya leo, Eduardo Mansur, amesema udongo ambao unahifadhi robo ya bayonuai na kuchangia asilimia 95 ya chakula, hivi sasa unakabiliwa na hatari kubwa.

Amesema ingawa mmomonyoko wa udongo unatokea katika maeneo yote, lakini kwa kiasi kikubwa unaweza kuchochewa kwa mara maelfu kutokana na kilimo kisichotumia mbinu endelevu na pia matumizi haramu ya ardhi ikiwemo ukataji miti kiholela.

“Mmomonyoko wa udongo  unaathiri afya ya udongo na tija katika uzalishaji kwa sababu unaondoa tabaka la juu la udongo wenye rutuba zaidi na kuacha udongo wa chini bila kizuio chochote,”  amesema Bwana Mansur.

Amesema hali hiyo inapunguza uzalishaji katika kilimo, inamomonyoa mzunguko wa bayonuai na kuchochea majanga yatokanayo na maji kama vile maporomoko ya udongo na mafuriko.

“Halikadhalika mmomonyoko wa udongo unaweza kuharibu miundombinu ya mijini na vijijini na katika hali mbaya zaidi husababisha watu kukimbia makazi yao,”  amefafanua Mkurugenzi huyo wa FAO.

Pamoja na mmomonyoko wa udongo kuwa tishio, Bwana Mansur ametaja pia mambo yanayotishia ustawi wenyewe wa udongo akisema ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha asidi na pia chumvi kwenye udongo, kupotea kwa bayonuai na kutoweka kwa hewa asilia ya ukaa kwenye udongo. 

Mmomonyoko wa udongo kupunguza mavuno kwa asilimia 10 ifikapo 2050

Kama hiyo haitoshi amesema kuwa iwapo kasi ya sasa itaendelea, mmomonyoko wa udongo unaweza kupunguza kiwango cha uzalishaji wa mazao kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2050.

“Hasara hii inamaanisha ni sawa na kuondoa mamilioni  ya hekta za ardhi ya kilimo. Kwa hiyo ni lazima tukomeshe mmomonyoko wa udongo ili kunusuru mustakabali wetu,” amesema Bwana Mansur akieleza kuwa, “unahitaji miaka 1,000 kupata sentimeta 1 ya tabaka la juu la udongo, lakini sentimeta hii moja ya udongo inaweza kupotezwa na mvua kubwa.”

Taka zinazochanganywa na kinyesi cha ng'ombe huwezesha wakulima kupata mboji ambayo ni kirutubisho cha udongo na mazao.
UNDP/Vietnam
Taka zinazochanganywa na kinyesi cha ng'ombe huwezesha wakulima kupata mboji ambayo ni kirutubisho cha udongo na mazao.

Tulinde vipi tabaka la juu ya udongo?

Bwana Mansur anaenda mbali kutaja ni kwa vipi basi mtu anaweza kulinda au kuzuia tabaka la juu la udongo akisema ni kwa, “wakulima na watumiaji wengine wa ardhi wanaweza kuanza kutumia mbinu bora za matumizi ya udongo katika mazingira ambayo yanaruhusu. FAO kwa upande wetu tuko tayari kuwasaidia.”

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter