Zaidi ya watu milioni 168 kuhitaji msaada wa kibinadamu 2020:OCHA

4 Disemba 2019

Watu zaidi ya milioni 168 kote duniani mwaka 2020 watahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi katika migogoro inayoendelea kwenye nchi Zaidi ya 50 limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu mimasuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA.

Akizindua ombi kwa wahisani la msaada wa dola karibu bilioni 29 hii leo  mjini Geneva Uswisi, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya kimataifa ya mtazamo wa masuala ya kibinadamu Mkuu wa OCHA Mark Lowcock amesema athari za mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa na vita vya muda mrefu vimesbabisha ongezeko kubwa la watu milioni 22 wanaohitaji msaada wa kibinadamu kwa mwaka jana.

Ameongeza kuwa, "mwaka 2020 karibu watu milioni 168 duniani kote watahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Hii inawakilisha takriban mtu mmoja kati ya watu 45 duniani, hii ni idadi kubwa kabisa katika miongo kadhaa”

Mwenendo mwingine unaotia hofu kwa mujibu wa Bwana Lowcock ni vita vya silaha ambavyo  amesema vinaua na kujeruhi idadi kubwa ya watoto.

Zaidi ya watoto 12,000 waliuawa au kujeruhiwa mwaka 2018 na mwaka 2019 umekuwa mbaya zaidi lakini pia vitendo vya ukatili na ubakaji kwa wanawake na wasichana .

Kuhusu mgawanyo wa fedha za msaada zitakazopatikana Lowcok amesema zitasaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.

Amesema kuwa, "Umoja wa Mataifa na mashirika wadau, shirika la msalaba mwekundu, mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s na washirika wengine tunaofanya nao kazi tutakuwa tunalenga kuwasaidia watu milioni 109 walio hatarini zaidi kupitia mipango 21 ambayo imeainishwa kwenye ripoti ya mtazamo wa kimataifa wa masuala ya kibinadamu. Msaada huo utahitaji ufadhili wa dola bilioni 29.”

Mkuu huyo wa OCHA maesema wanawake na wasichana walikuwa katika hatari kubwa ya ukatili wa kijinsia na kingono kuliko miaka ya nyuma na mtu 1 kati ya 5 wanaoishi katika maeneo yenye vita wana matatizo ya akili.

Hali halisi ya mahitaji

Amesema jamii nyingi zimeathirika na migogoro lakini nyingi zaidi zimeathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi kuliko ilivyotabiriwa hapo awali.

Amesisitiza kuwa ukame wa mara kwa mara , mafuriko na vimbunga vimekuwa kawaida na kuathiri kwa kiasi kikubwa watu masikini na wasiojiweza. “nchi 13 kati ya 20 vzilizo katika hatari ya athari za mabadiliko ya tabianchi ni maeneo ambako tumetoa ombi la msaada la mashirika mbalimbali ya kibinadamu.”

Na kuhusu ukubwa wa matatizo yanayohitaji msaada wa kibinadamu amesema “Yemen itasalia kuwa mgogoro mkubwa na mbaya zaidi duniani kwa mwaka 20202 baada ya miaka takriban 5 ya vita. Idadi ya watu wanaohitaji msaada inatarajiwa kusalia karibu ya kiwango cha mwaka huu ambacho ni karibu milioni 24 sawa na asilimia 80 ya watu wote.”

Ikifafanua kuhusu mgawanyo wa fedha hizo ripoti ya mtazamo wa masuala ya kibinadamu mwaka 2020 imesema kwa upande wa Yemen ombi ni dola bilioni 3.2. fedha pia zoinahitajika kwa ajili ya kusaidia kwenye migogoro mingine ya muda mrefu ikiwemo Afghanistan watu milioni 9.4 wanahitaji msaada na fedha zinazohitajika ni dola milioni 732.

Nchini Burundi ili kusaidia watu milioni 1.7 jumla ya dola milioni 104 zitahitajika, Iraq dola milioni 520 kwa ajili ya kuwasaidia watu milioni 4.1, Syria itahitaji dola bilioni 3.3 kwa ajili ya kuwahudumia watu milioni 11 na Jamhuri ya afrika ya Kati CAR itahitaji dola milioni 388 kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu milioni 2.6.

Ukiukaji wa sheria na haki

Akielezea jinsi wapiganaji wanavyoendelea kudharau sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu Lowcock amesema karibu mashambulizi 800 yamefanyika dhidi ya wahudumu wa afya na vituo vya afya katika miezi 9 ya kwanza yam waka 2019 ambayo yamekatili Maisha ya watu 171.

Ameongeza kuwa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza pia yamekuwa chachu kubwa ya kuongeza mahitaji ya kibinadamu kote duniani. “Afrika kwa mfano katika miezi mitatu ya mwaka huu kulikuwa na visa vya sulua asilimia 700 zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana wakati kama huo na kusababisha vifo Zaidi ya 5000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Akiigeukia Venezuela ambako ufadhili wa dola bilioni 1.35 unahitajika kwa ajili ya kunusuru Maisha ya watu milioni 3.8 mwaka 2020 lowcock amesema mahitaji yamepindukia uwezo wa rasilimali zilizopo.

Ameongeza kuwa msaada mkubwa unahitajika kwa ajili ya Wavenezuela walioko ndani ya nchi na pia takriban mara mbili ya msaada unahitajika kwa wale walioko nje ya nchi kusaka usalama na hifadhi.

Kwa mtazamo uliopo lowcock amesema “kwa mwenendo wetu wa sasa makadirio yanaonyesha kwamba Zaidi ya watu milioni 200 huenda wakahitaji msaada ifikapo mwaka 2022.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter