Je wajua kuwa ni nchi 1 tu kati  ya 5 ndio yenye mkakati wa afya wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi?

3 Disemba 2019

Ingawa binadamu anadhurika kwa kiasi kikubwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi bado serikali haziwezi mifumo ya kutosha kulinda afya za wananchi wao, limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO katika ripoti ya tathmini yake ya kwanza kabisa iliyotolewa hii leo ikimulika nchi 101.

WHO inasema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa mwiba kwa afya ya binadamu kutokana na kusababisha joto kupita kiasi, vimbunga na tsunami  lakini tathmini yao imeonesha kuwa ni nchi 1 tu kati ya 5 ndio ina mkakati wa afya kusaidia wananchi kukabiliana na  hali hizo.

Tathmini hiyo inaonesha kuwa watu wanafariki dunia kutokana na joto la kupindukia na pia majanga kama vile mafuriko na vimbunga.

Halikadhalika masuala ya uhakika wa chakula na upatikanaji wa maji, sambamba na magonjwa kama vile kipindupindu, dengue na Malaria.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus anasema kuwa, “mabadiliko ya tabianchi hivi sasa siyo tu yanasababisha gharama zitakazolipwa na vizazi vijavyo, bali pia ni gharama ambazo watu wanalipa hivi sasa kutokana na afya zao.”

Amesema ni kwa mantiki hiyo basi nchi lazima zitenge rasilimali zinazohitaji dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kulinda afya hivi sasa na za vizazi vijavyo.

Tathmini hiyo inaonesha kuwa watu wanafariki dunia kutokana na joto la kupindukia na pia majanga kama vile mafuriko na vimbunga - Ripoti

Madhara ni dhahiri lakini hakuna ushahidi wa hatua

Licha ya matokeo ya tathmini hiyo, asilimia takribani 60 ya mataifa husika yamesema kuna hatua finyu sana au hakuna kabisa katika kutenga rasilimali watu au fedha kwa ajili ya kuchukua hatua za kulinda afya za watu.

WHO inasema kuwa kuweka ajenda ya afya katika michakato ya kitaifa na kimataifa inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi kunaweza kusaidia kuelekeza fedha zinazohitajika.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa theluthi mbili ya michango ya kitaifa iliyotangazwa katika kukabili mabadiliko ya tabianchi kwa mujibu wa  mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi imetaja afya kama sehemu ya hatua za kukabili mabadiliko hayo lakini hakuna hatua za dhahiri katika utekelezaji.

Maisha ya watu milioni 1 yanaweza kuokolewa kwa kupunguza uchafuzi wa hewa pekee

Tafiti za awali za WHO zimebaini kuwa kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa mujibu wa mkataba wa Paris kunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kila mwaka duniani kote ifikapo mwaka 2050.

Hata hivyo WHO inasema kuwa mataifa mengi hayana uwezo wa kutumia fursa hiyo kama ilivyopendekezwa, takwimu zikionesha kuwa ni nchi 1 kati ya 44 inaweza kuonesha ushirikiano kati ya sekta ya afya na sekta muhimu zinazochochea mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa hewa kama vile sekta ya usafirishaji, uzalishaji umeme na nishati itumikayo majumbani.

Kwa upande mwingine, mataifa husika kwenye tathmini yalidhihirisha ushirikiano zaidi kati ya sekta ya afya na sera za mabadiliko ya tabianchi ambapo wamesema ushirikiano huo upo kwenye masuala ya maji, huduma za kujisafi na majitaka.

Sekta nyingine ni kilimo na huduma za kijamii.

Manufaa yatokanayo na kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa ni nadra zana kuakisiwa kwenye ahadi za kitaifa za tabianchi, imesema WHO ambapo ni nchi 1 tu kati ya 5 ndio zimetaja hoja ya afya kuhusiana na upunguzaji wa hewa chafuzi huko nchi 1 tu kati ya 10 ikitaja manufaa yanayotarajiwa kwenye sekta ya afya iwapo hewa chafuzi itapunguzwa.

“ili mkataba wa Paris uwe na manufaa kwa afya ya binadamu, serikali katika ngazi zote zinapaswa kupatia kipaumbele ujenzi wa mifumo ya afya iliyo na mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na nchi nyingi zinaelekea kwenye mwelekeo huo,” amesema Dkt. Maria Neira, Mkurugenzi wa Idara  ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Afya kwenye WHO.

Amesema kwa kuweka mfumo wa kujumuisha afya katika ahadi zilizotolewa kitaifa, NDCs katika kufanikisha mkataba huo, sambamba na mipango ya kitaifa ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi, mkataba wa Paris unaweza kuwa mkataba thabiti zaidi wa kimataifa kuhusu afya katika karne hii.

Nchi zilizoshiriki

Nchi 101 zilizoshiriki kwenye tathmini hiyo ni 27 kutoka ukanda wa Amerika, 13 kutoka Afrika, 20 kutoka Ulaya, 16 kutoka Mediteranea Mashariki,  17 kutoka ukanda wa pasifiki magharibi ilihali nchi 8 zimetoka kusini-mashariki mwa Asia.

 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter