Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utashi wa kisiasa ndio jawabu la kukabili mabadiliko ya tabianchi- Guterres

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterees akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Madris Hispania kabla ya kuanza kwa COP25 kesho Jumatatu .
UNFCCC
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterees akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Madris Hispania kabla ya kuanza kwa COP25 kesho Jumatatu .

Utashi wa kisiasa ndio jawabu la kukabili mabadiliko ya tabianchi- Guterres

Tabianchi na mazingira

Kuelekea kuanza kwa mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP25 huko Madrid, Hispania hapo kesho, hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari mjini humo na kueleza kuwa baada ya binadamu na sayari dunia kuwa katika mapambano hivi sasa dunia inajibu mashambulizi.

Bwana Guterres amesema kuwa hilo ni dhahiri kwa kuwa kipindi cha miaka mitano iliyopita imekuwa na kiwango cha juu cha joto cha kupindukia, “vina vya maji ya bahari ni vya juu kuwahi kufikiwa katika historia, theluji ikiyeyuka katika kasi isiyo ya kawaida na bahari zinakuwa na viwango vya juu vya asidi hali ambayo ina madhara makubwa kwa viumbe vya baharini.”

Katibu Mkuu amewaambia waandishi wa habari kuwa ripoti hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la hali ya hewa duniani, WMO ambayo itatolewa wakati wa mkutano huo akiendelea kuongeza kuwa, “majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianhi nayo yanazidi kushika kasi, yakiwa na madhara makubwa kupindukia huku yakigharimu uhai wa binadamu sambamba na gharama kubwa kifedha."

Gharama za mabadiliko ya tabianchi

“Kila mwaka, uchafuzi wa hali ya hewa unaohusiana na mabadiliko ya tabianchi huua watu milioni 7”, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi sasa ni kitisho kwa afya na usalama wa binadamu," amesema Katibu Mkuu.

Amesema kwa kifupi mabadiliko ya tabianchi hivi sasa si tishio la muda mrefu “bali tunakabiliwa hivi sasa na janga la tabianchi la dunia. Hivi sasa si wakati wa kugeuka nyuma kwa kuwa hali si shwari.”

Lakini tusikate tamaa bado tunaweza kuchukua hatua

Katibu Mkuu amesema kuwa ingawa hali inatisha, viwango vya joto vikipanda bado ujumbe wake siku ya leo ni wa matumaini na si wa kukatisha tamaa.

“Vita vyetu dhidi ya sayari dunia lazima vikome na tunafahamu kuwa hilo linawezekana. Wanasayansi wametupatia mwelekeo wa kufanikisha hilo,” amesema Bwana Guterres.

Amenukuu ripoti ya jopo la wataalamau wa kiserikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambalo lilisema kuwa lazima kudhibiti ongezeko la kiwango cha joto kisivuke nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi, uchafuzi wa hewa kutokana na hewa ya ukaa ukome ifikapo mwaka 2050 na kupunguza hewa chafuzi kwa silimia 45 kutoka viwango vya mwaka 2010 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo amesema hatua za kuweza kufanikisha mapendekezo hayo ya wataalamu bado hazitoshelezi.

“Ahadi nyingi zilizotolewa mjini Paris bado zinaweza kusababisha ongezeko la joto juu ya kiwango cha nyuzi joto 3, na bado nchi nyingi haziko hata katika mwelekeo wa kufikia ahadi hizo,” amesema Bwana Guterres.

Mathalani amesema kuwa hii leo dunia imejiandaa kuzalisha mafuta ya kisukuku kwa asilimia 120 zaidi kuliko kiwango kinachotakiwa ili kudhibiti joto katika nyuzi joto 1.5.

Na amesema kwa makaa ya mawe, kiwango cha uzalishaji ni asilimia 280.

 

Tweet URL

Hatua ni sasa, umma nao unapaza sauti tatizo hakuna utashi wa kisiasa

Lakini amesema kuwa ingawa hali ni hivyo bado jamii ya wanasayansi wanasema kuwa kuna uwezekano wa kudhibiti ongezeko la joto na zaidi ya yote, “teknolojia nazo pia zipo za kuweza kutusaidia.

Amesema kuwa umma nao haujakaa kimya kwani kila mahali unapaza sauti, vijana nao wakionyesha kuchukua hatua kila pahala wakiongoza na kuhamasisha hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kwamba miji mingi zaidi nayo inachukua hatua, taasisi za kifedha na wafanyabiashara nao wanaweka ahadi ya kudhibiti ongezeko la nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi.

Hata hivyo amesema kinachokosekana sasa ni utashi wa kisiasa, utashi wa kisiasa ambao utatoza hewa aya ukaa, utashi wa siasa utakaokomesha ruzuku katika nishati ya kisukuku na pia utashi wa kisiasa ambao utakoma kujenga mitambo ya makaa ya mawe kuanzia mwaka 2020.

“Lakini pia tunashuhudia kuwa wachafuzi wakubwa wa hewa duniani nao hawachukui hatua thabiti. Na bila wao lengo letu haliwezi kufikiwa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “ndio maana ni muhimu tunakutana hapa Madrid kwa COP25.“

Kwa mantiki hiyo, Guterres amesema, “natarajia kutoka hapa COP ni hatua thabiti za kutoa ahadi zinazotekelezeka na kuonyesha uwajibikaji na uongozi.”

Amesema katika miezi 12 ijayo ni lazima kuwa na ahadi thabiti za kitaifa hususan kutoka mataifa chafuzi ili kuanza kupunguza kabisa utoaji wa gesi chafuzi na kufikia lengo la kutokuwa na hewa ya ukaa chafuzi ifikapo mwaka 2050.

Katibu Mkuu amesema ana matumaini thabiti kuwa COP25 itakubaliana juu ya miongozi ya utekelezaji wa ibara ya 6 ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, kitendo ambacho kilishindwa kufikiwa huko Katowice wakati wa kupitisha kitabu cha kanuni cha utekelezaji wa mkataba wa Paris.

Mark Carney achukua 'mikoba' ya Bloomberg

Wakati huo huo, Katibu Mkuu Guterres amemteua Gavana wa sasa wa Benki Kuu ya Uingereza, Mark Carney, kuwa mjumbe wake maalum kwa masuala ya hatua kwa tabianchi.

Carney mwenye uraia wa Uingereza, Ireland na Canada amekuwa mstari wa mbele katika kusongesha sekta ya fedha katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Guterres amesema kuwa, "mjumbe huyo mpya atakuwa anajikita katika kutekeleza hatua hususan kuhamasisha uchangishaji wa fedha kuelekea kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzi joto 1.5."

Bwana anachukua nafasi ya mmarekani, Bwana Bloomberg ambaye sasa amejikita katika kuwania nafasi ya uraia wa Marekani.