Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukitaka mabadiliko katika hatua kwa tabianchi, lazima sisi tuwe mabadiliko- Guterres

Nishati  ya kisukuku ni moja ya visababishi vya hewa chafuzi zinazoongeza joto duniani
UN
Nishati ya kisukuku ni moja ya visababishi vya hewa chafuzi zinazoongeza joto duniani

Tukitaka mabadiliko katika hatua kwa tabianchi, lazima sisi tuwe mabadiliko- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza katika vikao mbalimbali mwanzoni mwa mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP25 hii leo huko Madrid Hispania na kusisitiza hatua thabiti na mshikamano katika kutekeleza makubaliano ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Guterres amesema mshikamano kama ulioonyeshwa na Chile na Hispania katika maandalizi ya mkutano huo ambao awali ulikuwa ufanyike Chile, ndio unaotakiwa pia katika kuondokana na dharura ya tabianchi.

“Tuko njiapanda katika juhudi zetu za kupunguza ongezeko la joto duniani. Mwishoni mwa muongo ujao tutakuwa katika njia moja kati ya njia mbili. Moja ni mwelekeo wa kujisalimisha ambao tumeupuuza hadi kufikia ukomo na kutia hatarini afya na usalama wa kila mtu kwenye sayari dunia. Je tunataka kukumbukwa kuwa kizazi kilichozika kichwa chake mchangani na kuwa kimya wakati dunia inateketea?” amehoji Katibu Mkuu wakati akifungua COP25.

Amesema njia nyingine ni ile ya matumaini, njia ya kuazimia kuwa na suluhu endelevu akisema kuwa, “njia ambayo nishati kisukuku itasalia ilipo, yaani ardhini, na njia ambako tutaelekea kuondokana na hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050. Hii ndio njia pekee ya kupunguza ongezeko la joto duniani ili lisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwishoni mwa karne hii.”

Tweet URL

Katibu Mkuu amesema fursa pekee ni COP25 kwa kuwa tayari wanasayansi wamezungumza juu ya madhara ya mabadiliko  ya tabianchi iwapo hatua hazitachukuliwa na kile kinachopaswa kufanyika ili kuepuka madhara zaidi.

Ametaka pia uraibu wa makaa ya mawe ukome sambamba na hatua endelevu za njia za usafirishaji, kilimo, mipango miji na ujenzi.

Tukitaka mabadiliko lazima sisi tuwe mabadiliko

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema, “iwapo tunataka mabadiliko lazima sisi tuwe mabadiliko. Kuchagua njia ya matumaini si jukumu la mtu mmoja, kiwanda kimoja au serikali moja pekee. Sote tupo katika hili. Mwelekeo uliowekwa bayana na wanasayansi uko bayana.”

Mwelekeo huo ni kwamba “ili kupunguza ongezeko la joto lisizidi nyuzi joto 1.5 ni lazima kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa asilimia 45 kutoka kiwango cha mwaka 2010 hadi ifikapo mwaka 2030 na tusizalishe kabisa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2030.”

Asiyesikia la mkuu huvunjika guu

Katibu Mkuu Guterres amekumbusha kuwa, “miaka 10 iliyopita, iwapo mataifa yangalichukua hatua ya kile yaliyochelezwa tungalitakiwa kupunguza uchafuzi kwa asilimia 3.3 kila mwaka, lakini hatukufanya hivyo. Hii leo tunatakiwa kupunguza kwa asilimia 7.6 ili tufikie lengo letu.”

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu amesema ni vyema serikali siyo tu zikatekeleza ahadi zao za kitaifa kwa mujibu wa mkataba wa Paris wa  mabadiliko ya tabianchi bali ziongeze ahadi.