Sekta ya kilimo ni muhimu katika kupunguza uchafuzi wa mazingira:FAO
Sekta ya kilimo ni muhimu katika kupunguza uchafuzi wa mazingira:FAO
Wakati mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP 25 ukianza leo huko Madrid Hispania shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesema sekta ya kilimo ni mchangiaji mkubwa wa ongezeko la joto duniani.
Shirika hilo limesema endapo dunia inataka kuahakikisha kiwango cha joto duniani hakizidi nyuzi joto 1.5 ifikapo mwisho wa karne hii , basi kupunguza uchafuzi wa gesi ya viwandani katika sekta ya kilimo ni muhimu sana.
Alex Jones , mkurugenzi wa idara ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira wa FAO anasema kilimo ni sehemu ya ajenda ya mabadiliko ya tabianchi na kuna changamoto kubwa ambazo zinahitaji ufumbuzi katika sekta hiyo ili kuhakikisha uchafuzi hauongezeki zikiwemo, "baadhi ni zile tunazoziita tathimini ya hasara na uharibifu, zininge zinahusu uhamishaji wa teknolojia ambayo imekuwa tatizo kubwa kuhusu endapo mataifa ya Kusini yanaweza kupata teknolojia wanayohitaji kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa kupewa iwe ni kwa masharti au bure, na tatizo kubwa kabisa ni kwamba nchi zote ziaztarajiwa kuwa na matamanio makubwa zaidi ya kupunguza hewa chafuzi, awali walisema kwa kiwango gani watapunguza uchafuzi huo lakini sasa kila mmoja yuko makini anataka kujipanga vizuri kwa sababu mwisho wa siku wanajua kuna athari kubwa.”
Kwa mujibu wa FAO sekta ya kilimo inachangia asilimia 24 ya hewa chafuzi je inapiga hatua yoyote katika kudhibiti hali hii? Alex anasema, "katika sekta chache kuna dalili dhahiri tunazoziita za kupunguza utoaji wa hewa chafuzi , mfano mzuri ni katika uzalishaji wa sekta ya maziwa . Sekta ya maziwa katika nchi nyingi imekuja na mkakati wa hiyari wa kupunguza hewa chafuzi kwa kila wanachozalisha na kujiwekea malengo ya kupunguza kiwango fulani kila mwaka . Hivyo kuna sekta zinalifanyia kazi hili na tunaona dalili njema . Na la muhimu zaidi ni suala hili kuwa katika ajenda , miaka mitatu au minne iliyopita kilimo hakikuwa katika ajenda ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi , sasa kila mtu anafahamu kwamba kilimo ndio kitovu cha suala hilo.”