Ni muhimu COP25 imalize sintofahamu ya ibara ya sita ya Mkataba wa Paris-Inger Andersen

Mahali unakofanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi COP25 mjini Madrid, Hispania
ifema feria de madrid
Mahali unakofanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi COP25 mjini Madrid, Hispania

Ni muhimu COP25 imalize sintofahamu ya ibara ya sita ya Mkataba wa Paris-Inger Andersen

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP25 ukianza hii leo mjini Madrid, Hispania, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Mpango wa mazingira wa Umoja wa Mataifa, UNEP Inger Andersen awali mjini New York Marekani kupitia mahojiano maalumu na UN News amesema moja ya vipaumbele vikuu vya mkutano huu itakuwa ni kufikia muafaka wa ibara ya sita ya mkataba wa Paris ambayo haikupata muafaka katika mkutano wa mwaka jana uliofanyika mjini Katowice Poland.

Ibara ya sita inayozungumziwa, ni ile inayohusu mfumo wa masoko ambao unazikubalia nchi kutimiza sehemu ya malengo yake ya ndani kupitia uuzaji wa hewa ya ukaa  ambapo mataifa yanakubaliwa kuuza sehemu yake ya utoaji wa hewa chafuzi. Bi Anderson anasema,“tunatambua kuwa kuna maoni tofauti lakini sasa ni wakati kufunga hiyo ibara, kuondoa mabano na kutafuta suluhisho ambalo linaweza kuunganisha kila mmoja pamoja.”

Akisisitiza zaidi kuhusu umuhimu wa ibara hiyo ya sita ya mkataba wa Paris, Mkurugenzi huyo Mkuu wa UNEP anasema,“hatuna muda. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliitisha mkutano wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mwezi Septemba na tulichoikiona pale ilikuwa nchi nyingi kujitokeza na kuongeza matarajio yao, hiyo ilikuwa vizuri, sasa tunahitaji hatua zaidi kufikia makubaliano katika ibara ya sita na kusonga mbele na matarajio na ahadi zaidi za kudhibiti hewa chafuzi.”

Mkurugenzi mkuu wa UNEP Inger Andersen, akihutubia mkutano mjini Nairobi, Kenya.
UNEP/Cyril Villemain
Mkurugenzi mkuu wa UNEP Inger Andersen, akihutubia mkutano mjini Nairobi, Kenya.

Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ingawa hauzifungi kisheria na wala hauziambii nchi jinsi zinavyopaswa kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi ili kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, lakini unazihimiza nchi kueleza ni nini wanaahidi kufanya, na ni kiasi gani wanapanga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Mkutano huu wa COP25 unaofanyika Madrid Hispania, unategemewa kudumu kwa wiki mbili hadi Ijumaa ya tarehe 13 mwezi huu.