Tumesikitishwa na uamuzi wa Mahakama kuu Israel:OHCHR

29 Novemba 2019

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema imesikitishwa na uamuzi wa mahakama kuu nchini Israel ya kukubaliana na uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kutomuongezea visa mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch kwa ofisi ya Israel na Palestina.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet jana amekutana na mkurugenzi huyo wa Human Rights Watch Omar Shakir ambaye alitakiwa kuondoka Israel Novemba 25 mwaka 2019 baada ya mahakama kuu kuafikia uamuzi wa serikali wa kutomuongezea visa.

Kamisha mkuu amesema amesikitishwa sana na uamuzi huo ambao ofisi ya haki za binadamu pamoja na wataalam maalum wa watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa pamoja waliitaka serikali ya Israel kuubadili kabla ya maamuzi ya mahakama kuu.

Kamishina Mkuu amesema, “kufukuzwa kwa bwana Shakir kunadhihirisha kivuli kinachoghubika ahadi za Israel katika utekelezaji wa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika, pamoja na uwezo wa watetezi wa haki za binadamu na mashirika kuendesha kazi zao za muhimu.”

Wataalam maalum wa hakiza binadamu wameeleza kwamba uhuru wa kujieleza na kujumuika unalinda na kusaidia uwezo wa kujieleza kwa makundi au upinzani hata wanaharakati na makundi ya vuguvugu kama BDS ambalo halichagizi ubaguzi, ghasia wala machafuko bali kudai haki.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter