Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ecuador chunguzeni madai ya mauaji na ukiukwaji wa haki:Bachelet

Mawio katika jimbo la Carchi nchini Ecuador (Septemba 2018)
WMO/Boris Palma
Mawio katika jimbo la Carchi nchini Ecuador (Septemba 2018)

Ecuador chunguzeni madai ya mauaji na ukiukwaji wa haki:Bachelet

Haki za binadamu

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet leo amewataka wadau wote nchini Ecuador kujihusisha na mazungumzo ili kuzuia migogoro mipya na kuunda jamii jumuishi na za amani kwa kuheshimu na kukumbatia mfumo wake wa tamaduni mbalimbali.

Kamishina Mkuu pia ametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru, wa haki, usio na upendeleo na wa wazi dhidi ya madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili uliotekelezwa Ecuador wakati wa maandamano ya tarehe 3 hadi 13 Oktoba yakijumuisha mauaji, ukiukwaji wa viwango na kanuni za kimataifa za matumizi ya nguvu, watu kuswekwa rumande pamoja na uporaji na uharibifu wa mali ya umma na binafsi.

Kufuatia mwaliko wa serikali ya Ecuador ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilituma ujumbe nchini humo kuanzia Oktoba 21 hadi Novemba 8 na Kamishina Mkuu ameushukuru uongozi wa nchi hiyo kwa taarifa zilizotolewa na mamlaka ya serikali na taasisi za umma kwa ujumbe wa haki za binadamu.

Lengo la ujumbe huo ilikuwa ni kukusanya taarifa na kubaini uwezekano wa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili uliofanyika katika wakati wa maandamano ambayo yalizuka kutokana na hatua za kubana matumizi kama vile kuondoa ruzuku kwenye Mafuta na baadhi ya mapendekezo ya masuala ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu timu hiyo ilikutana na maafisa kutoka pande zote za serikali, asasi za kijamii, makundi ya watu wa asili, waandishi wa habari, jumuiya, wahudumu wa sekta ya afya na wafanyabiashara.

Kwa ujumla watu 373 walihojiwa wakiwemo waathirika 83. Timu hiyo pia ilizuru vituo vitatu vya mahabusu na kufanya ziara mashinani majimbo ya Chimborazo, Tungurahua, Cotopaxi na Guayas.

Kutokana na taarifa zilizokusanywa na timu hiyo katika zaidi ya siku 11 za machafuko takriban watu tisa waliuawa na wengine 1,507 walijeruhiwa wakiwemo maafisa wa usalama 435 na watu wengine 1382 wamearifiwa kuswekwa rumande. Kamishina mkuu amesema, “machafuko ya mwezi uliopita yalikuwa na gharama kubwa kwa binadamu. Watu wanapaswa kuweza kuelezea madukuduku yao bila hofu ya kuumizwa wala kukamatwa na wakati huohuo ni muhimu kwamba waandamanaji wasijihusishe na ghasia.”

Timu hiyo ya haki za binadamu pia ilipokea taarifa kutoka kwa mashahidi na waathirika za matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa vikosi vya usalama ambayo yanakinzana na viwango na kanuni za kimataifa . Maafisa hao ni pamoja na polisi na jeshi.