Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake Sudan Kusini wasema sasa imetosha, waepushwe na ubakaji

Wanawake wakizungumza kwenye kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, Sudan Kusini. Kushoto ni Dudu Emilia.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Wanawake wakizungumza kwenye kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, Sudan Kusini. Kushoto ni Dudu Emilia.

Wanawake Sudan Kusini wasema sasa imetosha, waepushwe na ubakaji

Amani na Usalama

Siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake zikiendelea kuangaziwa duniani, nchini Sudan Kusini nako Umoja wa Mataifa umetumia kipindi hiki kutoa fursa kwa wanawake kupaza sauti zao huku ukimulika pia hatua za kuwawezesha kiuchumi wanawake hao. 

Mjini Juba, nchini  Sudan Kusini, maandamano yakiongozwa na Mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa nchini David Shearer akiambatana na wanawake na wanaume, kuashiria kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake wakipaza sauti sasa imetosha.

Dudu Emilia ni mmoja wa waandamanaji na mkazi wa Yei na anasema,  “tunapaswa kukomesha changamoto kama vile visa vya ubakaji, kwa sababu sisi wanawake ndio waathirika. Lazima wakomeshe na katu ubakaji usiendelee kwa sababu ukiendelea tutakuwa na maisha mabaya. Tuko hatarini, tunahitaji angalau tulindwe ili watoto wetu wawe na maisha ya furaha.”

Wakati wa vita vilivyoanza mwezi Disemba mwaka 2013, maelfu na wanawake na wasichana walibakwa. Achol Atem Nyinguut alilazimika kukimbia wakati wa mapigano lakini alibakwa na mwanaume mmoja aliyekuwa na silaha huku mtoto wake akitekwa nyara. Achol anasema kuwa,  “masahibu yalinipata kijijini kwetu. Na kijijini hakukuwepo na polisi au vituo vya polisi ili kuripoti.”

Achol ambaye ni mkazi wa Bor, hakuripoti kisa hicho na mtoto wake hadi leo hii hakupatikana. Hakupata  hata msaada wa matibabu na hadi sasa anaendelea kupata maumivu na hayuko peke yake kwenye machungu haya.

Kwa kutambua umuhimu wa kujengea uwezo wa kiuchumi wanawake, mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini kupitia tukio hili la ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS walionyesha kile wafanyacho kukwamua wanawake.

Miongoni mwa mashirika hayo ni lile la chakula na kilimo, FAO ambalo lilionyesha jinsi lilivyojengea uwezo wanawake kutengeneza majiko ya kupikia yasiyohitaji kuni, na hivyo kupunguza adha ya wanawake kwenda porini kusaka kuni, kitendo kinachowaweka hatarini kubakwa.