Heko Somalia kwa kuridhia kulinda wakimbizi wa ndani- UNHCR

27 Novemba 2019

Kitendo cha Somalia kuridhia mkataba muhimu wa kulinda wakimbizi wa  ndani barani Afrika ni mafanikio ya kihistoria kwa taifa hilo la pembe ya Afrika na bara zima la Afrika.

Hiyo ni kauli ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, kufuatia hatua ya Somalia kuridhia mkataba huo unaojulikana pia kama mkataba wa Kampala wa Muungano wa Afrika wa kuolinda na kusaidia wakimbizi wa ndani barani humo.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa tarehe 26 mwezi huu wa Novemba, Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed, “Farmaajo”, alitia saini mkataba huo baada ya kuridhiwa kwa kishindo kwenye Bunge la taifa hilo wiki iliyopita.

Hatua hiyo inafanya Somalia kuwa taifa la 30 barani Afrika kuridhia mkataba huo tangu upitishwe na Muungano wa Afrika mwaka 2009.

 “Kuridhiwa kwa mkataba wa Kampala unapatia msisitizo azma ya serikali ya kulinda mamilioni ya wakimbizi wa ndani Somalia na pia kusaka suluhu ya matatizo yao,” amesema Johann Siffointe ambaye ni Mwakilishi wa UNHCR nchini Somalia.

Kwa mantiki hiyo mwakilishi huyo amesema hii leo Somalia ni mfano wa kikanda kwa mataifa mengine kufuata na kwamba UNHCR ina ari ya kuendelea kusaidia serikali katika kutekeleza wajibu kwa mujibu wa mkataba huo.

UNHCR inasema hatua hiyo ya Somalia ni ya muhimu sana katika historia yake kwa kuzingatia kuwa ni ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.

Inadakiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 2.6 ni wakimbizi wa ndani Somalia.

Mwaka huu pekee wa 2019, zaidi ya watu 665,000 wamelazimika kukimbia makwao  nchini Somalia kutokana na mafuriko, mapigano na ukame.

Ingawa hivi sasa changamoto kubwa zinakabiliwa harakati za kuwapatia ulinzi wa kutosha, malazi, huduma za kujisafi, wakati huu ambapo wanakabiliwa na vitisho vya ukatili ikiwemo ule wa kijinsia.

Mkataba wa Kampala ulipitishwa mwaka 2009 na mataifa 55 ya Afrika na ni wa aina yake duniani na unaotambulika kisheria kikanda katika kulinda na kuwasaidia wakimbizi wa ndani.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter