Akiwa Sierra Leone, Ishmael aona moyo wa dhati wa wahudumu wa afya kunusuru uhai wa mtoto

27 Novemba 2019

Balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Ishamael Beah ametaka hatua zaidi zichukuliwe ili kulinda uhai wa watoto hususan wale wanaozaliwa njiti. 

Katika wadi ya watoto njiti kwenye hospitali  ya Ola During iliyoko mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, wanapata  mgeni, naye si mwingine bali ni balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Ishmael Beah. 

Mwenyewe akiwa raia wa Sierra Leone ambaye aliwahi kutumikishwa jeshini wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, anaonekana kustaajabu na kile anachoshuhudia.

Anapatiwa maelezo kuwa watoto hawa njiti kuna waliozaliwa katika hospitali hii na wengine wanaletwa baada ya kukosa huduma kwingineko ambako mama zao walijifungua wakati ujauzito una miezi sita na mtoto kuzaliwa akiwa na uzito wa chini ya nusu kilo. Alipata pia fursa ya kuzungumza na mama ambaye alijifungua mtoto njiti ambapo alizungumza naye kuhusu uzoefu wa mama huyo wa kupata mtoto njiti.

Uhai wa mtoto ni wa uhakika kutokana na uwepo wa mashine za kuwahifadhi ili watimize muda kamili wa kuzaliwa.

Ishmael akafunguka akisema, “nikiwa na mimi ni baba, ni vigumu sana kushuhudia hii. Nina watoto na ninavyoshuhudia hawa watoto, nafikiria pia watoto wangu. Unafahamu pale unapozaliwa na huduma unazopata ndivyo huamua mustakabali wa maisha yao. Nadhani kila mtu anapaswa kuwa na huduma kama hizi.”

Hata hivyo amesema, “pamoja na kuhuzunisha, inatia matumaini kuona madaktari na wauguzi hapa wanaojitolea kwa dhati, na bila shaka hawalipwi vizuri, lakini wanajitolea kwa moyo na si kwa malipo na wapo hapa kila siku kama uonavyo.”

Kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC, ambao mwaka huu umetimiza miaka 30, haki za mtoto zina misingi mikuu minne ambayo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter