Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ya kidijitali ndio mwelekeo sasa, twende nayo sambamba:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) akizungumza na wanafunzi wa shule ReDi inayojihusha na masuala ya kidijitali mjini Berlin, Ujerumani
UN Photo/Tobias Hofsaess
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) akizungumza na wanafunzi wa shule ReDi inayojihusha na masuala ya kidijitali mjini Berlin, Ujerumani

Teknolojia ya kidijitali ndio mwelekeo sasa, twende nayo sambamba:Guterres

Utamaduni na Elimu

Teknolojia ya dijitali ndio inayounda dunia hivi sasa na inakwenda kwa kasi isiyo ya kawaida hivyo kila mtu katika dunia hii anapaswa kwenda na kasi hiyo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo.

Akizungumza katika kongamano la kimataifa la udhibiti wa masuala ya intaneti mjini Berlin Ujerumani Guterres amesema “fursa ya upataji wa mtandao wa bure na wazi iko katika hatari, hatufanyi kazi kwa pamoja kuondoa mgawanyiko wa kijamii, kiuchumi na kisiasa. Lakini hili linaweza kubadilika. Na kuonyesha ni jinsi gani tunaweza kushirikiana mustakabali wa kidijitali kwa pamoja , vyema na kwa matarajio yetu sote.”

Katibu Mkuu ameonya kwamba endapo nchi hazitofanyakazi kwa pamoja kushughulikia pengo la fursa za kidijitali pamoja na migawanyiko yote ya kijamii na kisiasa inayochangiwa na pengo hilo, kizazi hiki kitakumbukwa kwa kuwa kile kilichosambaratisha ahadi ya awali ya intaneti.

Akianisha jukumu kubwa la intaneti katika kufikia mustakabali ulio sawia amesema “Kuwaunganisha watu wote duniani na mtandao wa intaneti ifikapo 2030 inapaswa kuwa kipaumbele chetu cha pamoja, sio tu kwa ajili ya maendeleo endelevu bali pia kwa usawa wa kijinsia.”

Mwaka huu ikiwa ni maadhimisho ya 30 tangu kubomolewa kwa ukuta wa Berlin mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezea taharuki yake kwamba “Sio tu tunajenga kuta zilizobayana zinazotenganisha watu lakini pia kuna hulka ya kujenga kuta zisizoonekana kwenye mtandao ambazo pia zinawatenga watu. Suluhu pekee ya janga hili ni mustakbali wa dunia moja, intaneti moja na mtazamo mmoja.”

Kuziba pengo la mgawanyiko

Katibu Mkuu amesema lengo la kuwa na fursa ya intaneti ambayo inapatikana, bure, salama na ya wazi kwa kila mtu liko katika hatari kubwa ya kuharibu mambo matatu muhimu ambayo ni mgawanyiko wa kidijitali, mgawanyiko wa kijamii na mgawanyiko wa kisiasa.

Kimataifa amesema watu wapatao bilioni 3.6 hawana fursa wanayomudu ya intaneti. Cha kushtusha zaidi mgawanyiko huu unawaathiri zaidi watu walio katika nchi zenye maendeleo duni ambako mtandao wa intaneti ungeweza kuwa na mabadiliko makubwa chanya. Wakati huo huo ameongeza kuwa pengo la kijisinsia katika kuunganishwa na mtandao wa kidijitali linaendelea kupanuka.

Duniani kote takriban watu milioni 327, wanawake wachache kuliko wanaume ndio wenye simu za kisasa za rununu na wanaweza kupata mtandao wa intaneti. Wanawake pia ndio walio idadi ndogo sana katika uwakilishi wa kazi za sekta ya Habari na mawasiliano, nyadhifa za juu za utawala, na  kazi za wanazuoni katika sekta ya teknolojia. Na asilimia 90 ya watu wanaosaka mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara imebainika kuwa ni wanaume.

Bwana Guterres amesema pengo la kidijitali linaweza kuchochea migawanyiko zaidi ya kijamii.

Kuzama kwenye mtandao

Katibu Mkuu amesema “Imani yangu ni kwamba intaneti inaweza kuwa nyenzo yenye nguvu sana kwa kufanya yaliyo mema, lakini tunaona pia kwamba inaweza kuwa ni nyenzo ambayo inaweza kutumika katika mambo mabaya.

Utando unaotathimini masuala ya mitandao ya kijamii unaweza kututumbukiza sote katika jungu la maoni yetu wenyewe na hulka zetu. Hivi sasa masuala ya kisiasa na jamii kwa ujumla vinashawishiwa na sekta kubwa ya mitandao ya kkijamii isiyodhibitiwa huku akili bandia ikitumika kurubuni wapiga kura, kuwasaka watetezi wa haki za binadamu na kunyamazisha upinzani.

Amesisitiza kwamba “tunahitaji pia kuelewa uhusiano baida ya maendeleo ya kidijitali na kutokuwepo na usawa. Tunajua kwamba kutokuwepo usawa na kubagua kunachochea machafuko ya kijamii na vita. Pia tunafahamu kwamba teknolojia kufuatana na matumizi yake inaweza kuwa chachu ya kuongeza pengo la kijamii au kuolipunguza . Na mgawanyiko wa kisiasa unaweza kuleta tishio kubwa katika biashara, usalama na mifumo ya intaneti.