Bila kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa kwa asilimia 7.6 lengo la nyuzi joto 1.5 halitafikiwa-Ripoti ya UNEP

26 Novemba 2019

Katika kuelekea mwaka ambao mataifa yataimarisha ahadi zao za ulindaji wa hali ya hewa zilizoafikiwa mjini Paris, ripoti mpya iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi na shirika la Mpango wa mazingira wa Umoja wa Mataifa, UNEP, imeonya kuwa, ulimwengu utashindwa kufikia lengo la nyuzi joto 1.5 la mkataba wa Paris ikiwa dunia haitapunguza hewa chafuzi kwa asilimia 7.6 kila mwaka kati ya mwaka 2020 na 2030.

Ripoti hiyo ya mwaka ya UNEP inasema kuwa hata kama ahadi zote za sasa chini ya mkataba wa Paris zitatekelezwa, joto linategemewa kuongezeka kwa nyuzi joto 3.2, na kuongeza madhara zaidi ya hali ya hewa hivyo matamanio zaidi ya pamoja yanatakiwa kuongezeka zaidi ya mara tano juu ya viwango vya sasa ili kufikia punguzo linalotakiwa kwa muongo ujao la nyuzi joto 1.5.

2020 ni mwaka muhimu wa hatua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ambapo kutakuwa na mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabiachi mjini Glasgow, Scotland ukilenga kuamua mstakabali wa siku zijazo wa juhudi za kudhibiti janga, na nchi zinatarajiwa kuongeza ahadi zao kuhusu kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema, "kwa miaka kumi, ripoti za uchafuzi wa hewa zimekuwa zikitahadharisha na kwa miaka kumi ulimwengu umeongeza uchafuzi. Hakuna wakati uliokuwa muhimu zaidi kuisikiliza sayansi kaama wakati huu. Kushindwa kufuata maonyo haya na kuchukua hatua kali za kudhibiti uchafuzi, ina maana tutaendelea kushuhudia mawimbi makali na mabaya ya joto, vimbunga na mmonyoko.”

Na katika kuonesha ukubwa wa tatizo la sasa, Inger Andersen, Mkurugenzi mkuu wa UNEP amesema, “tunafahamu kuwa katika nyuzi joto 1.5, asilimia 75 ya matumbawe yatakufa, na katika nyuzi joto mbili matumbawe yatatoweka kabisa. Tunaelewa kuwa wadudu ambao tunawahitaji kwa ajili ya uchavushaji ili kutengeneza chakula chetu wataathirika sana na kuna uwezekano wa kupoteza makazi na hivyo wadudu nao kwa kiwango cha juu.”

Jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC imeshaonya kuwa kwenda zaidi ya nyuzi joto 1.5 kutaongeza idadi ya ukubwa wa majanga ya mabadiliko ya tabianchi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter