Kila saa 1 watoto na barubaru 13 wanafariki dunia, kisa? UKIMWI, UNICEF yataka hatua zaidi.

Lightom mtoto wa umri wa mwaka mmoja akipokea dawa za kupunguza makali ya ukimwi nyumbani kila siku katika eneo la Mbarara Uganda.
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Lightom mtoto wa umri wa mwaka mmoja akipokea dawa za kupunguza makali ya ukimwi nyumbani kila siku katika eneo la Mbarara Uganda.

Kila saa 1 watoto na barubaru 13 wanafariki dunia, kisa? UKIMWI, UNICEF yataka hatua zaidi.

Afya

Watoto na barubaru zaidi ya 300 hufariki dunia kila siku , sawa na 13 kila saa kwa sababu zinazohusiana na masuala ya ukimwi, na nusu tu ndio wanaopata matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Ripoti hiyo ya kimataifa inayomulika virusi vya ukimwi VVU na ukimwi imetolewa leo mjini Geneva Uswis na inasema kutokuwepo na fursa za kutosha za matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi na juhudi ndogo za kuzuia maambukizi mapya ndio sababu kubwa za vifo hivi, huku kukiwa na asilimia 54 ya watoto wa umri wa kati ya sufuri hadi miaka 14 waliobainika kuishi na VVU kwa mwaka 2018 au 79,000 wanaopata huduma ya matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore"ulimwengu uko kwenye azma ya kupata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya VVU na Ukimwi, lakini hatupaswi kupumzika kutokana na mafanikio haya yaliyopatikana. Kupuuza vipimo na  mikakati ya matibabu kwa Watoto na barubaru ni suala la uhai na kifo na kwa kwao ni lazima tuchague maisha. "

Hali halisi ya huduma

Takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha kuna tofauti kubwa kikanda za fursa za kupata matibabu miongoni mwa watoto wanaoishi na VVU. Fursa ni kubwa zaidi katika nchi za Asia zikiwa katika kiwango cha asilimia 91 zikifuatiwa na Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini asilimia 73, Mashariki na Kusini mwa Afrika  pamoja na Asia Mashariki na Pasifiki asilimia 61, Amerika ya Kusini na Karibea asilimia 46 na kiwango cha chini zaidi kikiwa Magharibi na Katikati mwa Afrika ambako ni asilimia 28.

Pia ripoti inasema fursa ya kina mama wajawazito kupata dawa za kuzuia maambuziki kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto imeongezeka kimataifa na kufikia asilimia 82 kutoka asilimia 44 chini ya miaka 10 iliyopita .

Hata hivyo ripoti inasema bado kuna tofauti kubwa miongoni mwa kanda ambapo Mashariki na Kusini mwa Afrika kukiwa na fursa kubwa ya asilimia 92 ikifuatiwa na Amerika ya Kusini na Karibea asilimia 79 na Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini zikiwa na asilimia ndogo katika hili.

Wakati tukiwa bado na safari ndefu kuwapa zaidi kina mama wajawazito matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kumesaidia kuepusha maambukizi mapya takriban milioni 2 ya VVU na kuzuia vifo zaidi ya milioni 1 vya Watoto wa umri wa chini ya umri wa miaka 5. Tunahitaji kuona matibabu sawa na hayo pia kwa Watoto. Kuziba pengo hili baina ya watoto na mama zao kutaongeza kwa kiasi kikubwa umri wa watu kuishi na ubora wa maisha ya watoto walioathirika na VVU.”

Takwimu za maambukizi.

Ripoti inasema kwamba mwaka 2018 takriban watoto 160,000 wa umri wa kuanzia 0 hadi miaka 9 walipata maambukizi mapya ya VVU na hivyo kufanya idadi ya watoto wa umri huo wanaoishi na VVU kufikia milioni 1.1.

Watoto wengine 89,000 wa chini ya umri wa miaka 5 waliambukizwa wakati wa ujauzito au wa kujifungua  na wengine 76,000 waliambukizwa wakati wa kunyonyeshwa kwa mwaka 2018. Pia mwaka huohuo wasichana barubaru 140,000 walipata maambukizi mapya ya VVU ikilinganishwa na wavulana barubaru 50,000.

Kinachopaswa kufanyika

Ili kutokomeza ukiwmi kama tishio kubwa la afya ya umma kwa mustakbali wa vizazi vjavyo UNICEF imezitaka serikali na wadau wote kuboresha huduma za upimaji na takwimu za matibabu kwa watoto na barubaru, ili kuwreza kukabiliana vyema na mahitaji ya kundi hilo lililoko hatarini. Pia imetaka kuwepo na uwekezaji na kutekeleza kikamilivu mikakati bunifu ya kuziba haraka pengo la upimaji na matibabu kwa watoto na barubaru wanaoishi na VVU.

Mkuu wa UNICEF Bi. Fore amesisitiza kuwa “Gharama ya kushindwa kupima na kutibu kila mtoto aliyeko katika hatari ya VVU ni ile tunayoipima katika maisha na mustakbali wa watoto, gharama ambayo hakuna jamii inayoweza kuimudu. Miradi ya VVU inahitaji kufadhiliwa kikamilifu na kuwezeshwa , kuhifadhi, kulinda na kuboresha maisha kwa ajili ya watoto katika muongo wa kwanza na wa pili.”