Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde jamii ya kimataifa igeukieni Sudan- Lowcock

Mark Lowcock, (kulia) Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu wakati wa ziara  yake Sudan Kusini, na pichani akizungumza na mmoja wa wahudumu wa afya katika hospitali ya mafunzo ya Kassala
OCHA/Saviano Abreu
Mark Lowcock, (kulia) Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu wakati wa ziara yake Sudan Kusini, na pichani akizungumza na mmoja wa wahudumu wa afya katika hospitali ya mafunzo ya Kassala

Chonde chonde jamii ya kimataifa igeukieni Sudan- Lowcock

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock amehitimisha ziara yake nchini Sudan akitaka jamii ya kimataifa iongeze kasi ya kupeleka misaada ya kibinadamu nchini humo.

Bwana Lowcock katika ziara yake ya kwanza tangu kuundwa kwa serikali ya mpito nchini humo mwezi Agosti mwaka huu, ameshuhudia kudorora kwa hali ya kibinadamu hususan kwenye maeneo ya kati na mashariki mwa nchi hiyo akisema kuwa mamilioni ya maisha ya watu yako hatarini.

Mathalani akiwa jimbo la Kassala, mashariki mwa Sudan, amejionea hali halisi ambako, zaidi ya watu 400,000 wanakabiliwa na uhaba wa chakula na ni asilimia 13 tu ya wakazi wa vijijini ndio wanapata huduma ya maji safi na salama, milipuko ya magonjwa nayo ikikwamisha harakati za serikali za kuchukua hatua kusaidia kukwamua jamii.

Bwana Lowcock amesema kuwa, “hapa hakuna mzozo. Kuna amani na utulivu na kihistoria mashirika ya misaada ya kibinadamu huwa hayafiki huku. Lakini sasa kuna janga la kiuchumi, na kuna tatizo la utapiamlo. Kuna mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yanayoua kama vile kipindupindu, dengue, surua na donda koo.”

Mkuu huyo wa OCHA pia amekutana na Waziri Mkuu Abdallah Hamdock ambapo amesema, “kuna serikali mpya Sudan na ina ajenda ya maendeleo. Hata hivyo inahitaji msaada zaidi kutoka jamii ya kimataifa. Tunatarajia miezi michache ijayo kushuhudia tatizo la kibinadamu hapa, hata katika maeneo yenye amani”

Bwana Lowcock amepongeza azma ya Sudan ya kuongeza uwezo wa mashirika kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wahitaji huku akitambua hatua zilizochukuliwa hadi sasa ikiwemo kupunguza taratibu za kiutawala kuruhusu mashirika hayo.

Yaelezwa kuwa serikali ya Sudan pia inasaidia juhudi za kuwezesha mashirika ya misaada kupita maeneo ambayo bado yako chini ya vikundi vilivyojihami huku Bwana Lowcock akipongeza pia kipaumbele cha serikali ya Sudan katika ujenzi wa amani na kusuluhisha mizozo nchini humo.

Hivi sasa nchini Sudan zaidi ya watu milioni 8.5 wanahitaji misaada ya chakula, lishe, ulinzi na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Mzozo nchini Sudan umesababisha takribani watu milioni 2 kusalia wakimbizi wa ndani huko  Darfur, Kordofan Kusini na eneo la Blue Nile.