Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa jamii Sudan Kusini na UNMISS walaani vurugu dhidi ya raia na walinda amani

Bentiu ni kambi kubwa zaidi ya kulinda raia nchini Sudan Kusini
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Bentiu ni kambi kubwa zaidi ya kulinda raia nchini Sudan Kusini

Viongozi wa jamii Sudan Kusini na UNMISS walaani vurugu dhidi ya raia na walinda amani

Amani na Usalama

Viongozi wa kijamii nchini Sudan Kusini wameomba radhi kwa vitendo vya ghasia vilivyofanywa na vijana waliokuwa wamelewa katika kambi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda raia mjini Bentiu ambapo raia wawili walifariki dunia na wafanyakazi wanane wa Umoja wa Mataifa kujeruhiwa wakiwemo maafisa wa polisi watano.

Kupitia taarifa iliyotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa vyombo vya Habari hii leo, ni kuwa  ujumbe kutoka chama cha Sudan People’s Liberation Army, SPLA, walikutana na viongozi wa jamii katika kambi ya kulinda raia mapema jana. Waliwasihi vijana kutojihusisha na ghasia dhidi ya watu wengine waliofurushwa kutoka kwenye makazi yao na pia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wakaahidi kusaidia juhudi za kuwawajibisha waliohusika.

Mapigano yalizuka kati ya makundi ya vijana wadogo wa kiume walevi katika kambi mnamo tarehe 21 ya mwezi huu wa Novemba. Wakati maafisa wa polisi wa Umoja wa Mataifa walipoingilia kati ili kuzuia vurugu hizo na kuwalinda raia, vijana waliwageukia maafisa hao na kuanza kuwarushia mawe na pia kuwapiga kwa fimbo.

Ijumaa, wafanyakazi wa kiraia wa Umoja wa Mataifa, ili kueleza maskitiko yao na salamu za rambirambi, walitembelea familia ya kijana mmoja ambaye alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na tukio hilo la alhamis. Wakati kikao na familia kikiendelea, kundi la vijana walivamia magari ya UNMISS, ikiwemo kuliteketeza gari moja kwa moto. Pia vijana hao walishambulia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wakimpiga mmoja kwa fimbo na kumkata mwingine kwa mkuki.

Vijana pia waliwageukia walinda amani kutoka Ghana ambao walijaribu kuingilia tukio hilo, wakiwarushia mawe, mikuki na mabomu ya petrol ambapo bomu moja lililipiga gari na kuliteketeza kwa moto. Vijana hao pia walijaribu kuwanyang’anya silaha walinda amani na walifanikiwa kuharibu vituo viwili vya ulinzi. Risasi mbili zilifyatuliwa hewani ili kuwatawanya waandamanaji.

UNMISS inafanya uchunguzi kuhusu ghasia hizo ikiwemo vifo vya vijana wawili waliohusika.Viongozi wa kijamii wanasaidia katika mchakato huo.

Kambi za kuwalinda raia nchini Sudan Kusini zilianzishwa mnamo mwaka 2013 ili kuwapatia hifadhi raia wanaokimbia vurugu baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza. Taarifa ya UNMISS imeonya kuwa haikubaliki kwa wanajamii kujihusisha katika vurugu miongoni mwao na hata dhidi ya  walinda amani ambao wanafanya kila waliwezalo kuwapatia ulinzi familia zilizoko katika  mazingira hatarishi.