Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kundi la tatu la wakimbizi wanaoondolewa Libya lawasili Rwanda:UNHCR

Kundi la baadhi ya wakimbizi 116 ambao wamewasili katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali kufuatia kuhamishwa nchini Libya.
©UNHCR/Eugene Sibomana
Kundi la baadhi ya wakimbizi 116 ambao wamewasili katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali kufuatia kuhamishwa nchini Libya.

Kundi la tatu la wakimbizi wanaoondolewa Libya lawasili Rwanda:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kundi la tatu la wakimbizi zaidi ya 100 wakiwemo watoto wachanga waliozaliwa kwenye vituo vya kushikilia wakimbizi na wahamiaji nchini Libya limewasili Rwanda kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa UNHCR kundi hilo lililo na jumla ya wakimbizi 116 liliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kigali Jumapili usiku na kupelekwa kwenye kituo cha muda cha Gashora ambako UNHCR inawapa msaada wa kuokoa maisha ikiwemo chakula, maji, huduma za afya , msaada wa kisaikolojia na malazi.Mwakilishi maalum wa UNHCR katika ukanda wa Mediterranea ya Kati Vincet Cochetel amesema "wakati ghasia zikishika kasi mjini tripoli uhamishaji huu wa wakimbizi ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote, lakini kukiwa bado na maelfu ya wakimbizi walio katika hatari  kwenye vituo mbalimbali na maeneo ya mijini nchini Libya tunahitaji nchi kutusaidia kuwaondoa wakimbizi zaidi kutoka Libya haraka iwezekanavyo. "

Kundi hili la tatu la wakimbizi wengi wao wanatoka Eritrea na wengine wachache kutoka Somalia, Ethiopia, Sudan na Sudan Kusini.

UNHCR inasema takriban theluthi mbili ya wakimbizi hao waliowasili wako chini ya umri wa miaka 18 na wengi wao wametangana na wazazi au walezi wao na kuna Watoto wawili walio na umri wa mwezi mmoja.

Vijana watatu wakimbizi wakisubiri katika uwanja wa ndege wa Kigali Rwanda baada ya kuhamishwa kwa njia ya ndege kutoka Libya.
©UNHCR/Eugene Sibomana
Vijana watatu wakimbizi wakisubiri katika uwanja wa ndege wa Kigali Rwanda baada ya kuhamishwa kwa njia ya ndege kutoka Libya.

 

Kwa sasa watu hao wamepewa hadhi ya waomba hifadhi wakati kesi zao zikifanyiwa tathimini  na kisha kupatiwa suluhu, ikiwemo makazi, kujerea nyumbani walikotoka au walikokuwa wakiishi kwa hiyari kama kutakuwa salama kufanya hivyo na kuwajumuisha katika jamii Rwanda.

Ndege zingine za msaada wa kibinadamu zinatarajiwa kwenda Libya kuwahamisha wakimbizi wengine katika wiki chache zijazo.

Karibu wakimbizi na waomba hifadhi 4500 bado wanashikiliwa katika vituo mbalimbali nchini Libya ikiwemo wale waliokamatwa tena baada ya kuokolewa hivi karibuni kwenye mwambao wa Libya.