Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Afghanstan yalaani vikali kuuawa kwa afisa wake katika shambulio

Picha ya Maktaba ikionesha sehemu ya mji wa Kabul, Afghanstan
UNAMA/Freshta Dunia
Picha ya Maktaba ikionesha sehemu ya mji wa Kabul, Afghanstan

UN Afghanstan yalaani vikali kuuawa kwa afisa wake katika shambulio

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa nchini Afghanstan kwa maskitiko makubwa umethibitisha kuuawa kwa afisa wake mmoja wa kigeni na wengine wawili kujeruhiwa katika shambulizi lililolilenga Gari la Umoja wa Mataifa usiku wa kuamkia leo jumapili mjini Kabul.

"Rambirambi zetu ziwafikie wana familia wa mwenzetu." imeeleza taaria ya awali.

Hakuna taarifa za ziada kuhusu afisa huyu wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa aliyepoteza maisha akiwa Afghanstan na bado taarifa za waliojeruhiwa akiwemo mfanyakazi mwingine wa kigeni na mwenyeji hazijawekwa wazi lakini taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema itaziweka wazi muda mfupi ujao.

"Umoja wa Mataifa unalaani vikali shambulizi hilo." Imesisitiza taarifa.

Vyombo vya habari vinadai hakuna kundi lolote ambalo limejihusisha na shambulizi hili.

Umoja wa Mataifa nchini Afghanstan umetoa wito kwa mamlaka za Afghanstan kufanya uchunguzi wa kina kuhusu shambulizi hili na kuwafikisha katika mikono ya sharia waliohusika kulitekeleza.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mara baada ya kuipokea taarifa hiyo, ametoa taarifa ya maskinitiko kupitia msemaji wake akitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza mwanafamilia na pia kuwatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa.

Aidha, Katibu mkuu Guterres amezitaka mamlaka za Afghanstan kuhakikisha wanawatambua na kuwafikisha katika mkono wa sheria waliotekeleza shabulizi hilo dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Umoja wa Mataifa.