Mahitaji ya kibinadamu Sudan ni makubwa na yanatia hofu:Lowcock

22 Novemba 2019

Mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan ni makubwa na yanachangiwa na sababu mbalimbali amesema mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA.

Mark Lowcock ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza kabisa Sudan tangu kuanzishwa serikali ya mpito Sudan mwezi agosti mwaka huu amesema miongoni mwa sababu hizo ni mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa na mgogoro wa kiuchumi.

Ameongeza kuwa watu zaidi ya milioni 8.5 wakiwemo wakimbizi wa ndani milioni 1.9 wanahitaji msaada wa kibinadamu na mahitaji yao yanatarajiwa kuongezeka.

Bwana Lowcock amesema hivi sasa kinachotoa hifu kubwa ni milipuko ya magonjwa inayoendelea  na imechochewa na mafuriko ya hivi karibuni ambayo ni mabaya zaidi tangu mwaka 2013, kwani maji yaliyotuama yamekuwa chachu kubwa ya magonjwa yatokanayo na maji na pia mazalia ya mbu.

Wizara ya afya ya Sudan wiki hii imetangaza mlipuko wa homa ya bonde la ufa ambapo hadi sasa kumeripotiwa visa 319 vinavyoshukiwa ikiwemo vifo 11.

Kwa mujibu wa OCHA vikosi kazi maalum vimeanmzishwa katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwenye majimbo ya Bahari ya Sham na Mto Nile.

Pia shughuli za kudhibiti kusambaa kwa wadudu zinaendelea kwa ukaguzi majumbani na kupuliza dawa za kutokomeza mbu.

Mkuu wa OCHA amesema moja ya kipengee cha mgogoro wa kiuchumi kinachowaathiri watu wasiojiweza moja kwa moja ni bei ya chakula ambayo badi ni ya juu sana au karibu inavunja rekodi licha ya kuwa na mwaka mzuri wa mavuno mwaka jana na kuwa na matumaini ya msimu mzuri mwaka huu.

Akitolea mfano amesema mathalani mwezi Oktoba mwaka huu bei ya mtama kwenye masoko mjini Khartoum ilikuwa mara tano zaidi ya mwezi Oktoba mwaka 2017.

Hata hivyo Bwana Lowcock amesema ili kuisaidia hatua za kitaifa kukabiliana na hali hiyo makundi ya misaada kote nchini yanachukua hatua kusaidia chini ya mwamvuli wa mpango wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa, na mpango huo unahitaji dola bilioni 1.1 za ufadhili na hadi sasa umefadhiliwa asilimia 51 pekee.

 

TAGS: Sudan, mabadiliko ya tabianchi, Mark Lowcock, wakimbizi wa ndani, msaada wa kibinadamu, OCHA

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter