Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kifo cha mtu mmoja aliyekuwa na ebola chazua tafrani kwa jamii nchini DRC

Waathirika wa ugonjwa wa ebola wamezikwa katika makaburi ya eneo la Kitatumba, Butembo mashariki mwa DRC. (Agosti 2019)
UN Photo/Martine Perret
Waathirika wa ugonjwa wa ebola wamezikwa katika makaburi ya eneo la Kitatumba, Butembo mashariki mwa DRC. (Agosti 2019)

Kifo cha mtu mmoja aliyekuwa na ebola chazua tafrani kwa jamii nchini DRC

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC kumeripotiwa wagonjwa wapya saba wa ebola waliothibithishwa katika kipindi cha wiki moja iliyomalizika tarehe 19 mwezi huu wa Novemba katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO.

Baada ya siku thelathini bila kuripotiwa kwa mgonjwa yeyote wa ebola katika eneo la Oicha, katika wiki moja iliyomalizikia Jumanne wiki hii mgonjwa mpya ameripotiwa na kufariki dunia na kuelezewa kuwa ni sawa na kifo cha jamii.

Dkt. Mike Ryan, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa WHO akihusika na programu za afya ya dharura amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa,“Mtu huyu ambaye amegeuka kuwa kifo kwa jamii alikuwa ametembelea vituo vitatu tofauti katika eneo la Oicha kabla ya kugundulika alikuwa ni mwendesha pikipiki na wakati waendesha pikipiki wenzake katika kundi hilo walifahamu kuhusu kifo chake walikuja kutoa rambirambi zao na mwili wake kusogelewa na  marafiki wengi na waendesha pikipiki wenzake.. Hii ni jamii ambayo wanasafiri na wengi wao wameenda sehemu nyingine kwa mfano Kalanguta na kwingineko.”

WHO imesema kwa kuzingatia kisa hicho kimoja tu ni kwamba sasa hivi kuna zaidi ya watu 200 ambao wamehusishwa na kisa hicho huku watu 62 wakitajwa kuwa katika hatari zaidi na kwamba,“Sasa tuna hali ambayo tuna maambukizi katika eneo ambako kuna mapigano. Hakuna mtu aliyetarajia hicho. Kwa hivyo kwa sasa kila mtu anapaswa kuzingatia hilo na kusema , ni nini tunaweza kufanya ili kuweka mazingira ambamo utoaji wa huduma utaendelea na hiyo inahitaji hatua kutoka kwa kila mtu, kutoka kwa serikali, MONUSCO, Umoja wa Mataifa na kila mtu.”

Hata hivyo Dkt. Ryan amesema kufikia sasa wamepiga hatua kubwa katika kudhibiti ebola katika kipindi cha miezi miwili au mitatu na kwamba tukio hili linaloshuhudiwa ni fursa kwa wadau kumaliza kazi ambayo imekuwa ikiendelea.

Kufikia tarehe 19 mwezi huu wa Novemba, wagonjwa 3298 wameripotiwa ambapo kati yao hao, 3180 wamethibitishwa kuwa na ebola ilhali 118 wanashukiwa huku  kati ya hao, wagonjwa 2197 wamefariki dunia.