Shambulio la makombora lasababisha raia 12 kuuawa Idlib, Syria UN yataka uchunguzi ufanyike

21 Novemba 2019

Mzozo nchini Syria unaendelea kuua na kujeruhi raia huku ripoti zikisema  ufyatuaji wa makombora kwenye kwa makazi ya watu wanaokimbia machafuko katika maeneo ya kaskazini magharibi siku ya  Jumatano usiku, umesababisha watu 12 kupoteza maisha na makumi wengine ikiwemo watoto kujeruhiwa, yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu hii leo.

Akizungumza na waandhishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Fran Equiza amesema, “ripoti za mashambulizi karibu na kambi ya wakimbizi wa ndani ya Qah karibu na mpaka wa Uturuki huko Idlib usiku wa jana yamesababisha uharibifu katika hospitali ya wazazi.” Ameongeza kwamba, “watoto ni miongoni mwa waathirika; ambako pia kambi za wakimbizi wa ndani jirani ziliharibiwa.”

Kwa upande wake Naibu Mratibu wa misaada ya kibinadmu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda kwa ajili ya mzozo wa Syria, Mark Cutts ametoa wito kwa uchunguzaji wa kitendo hicho alichosema ni cha kutisha.

Ameongeza kwamba, “naghadhabishwa na kwamba makombora yalilenga raia ikiwemo wazee, wanawake na watoto waliokuwa katika vyandarua kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani.”

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA katika taarifa yake imelaani uwepo wa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na wafanyakazi wake nchini Syria.

Bwana Cuts amesisitiza kwamba, “sheria ya kimataifa inasema kwamba pande husika zinahitaji kutofautisha kati ya raia na makundi yaliyojihami na kuzingatia kwamba wanawaepusha raia kutoka kwa operesheni za kijeshi.”

Watoto ni waathirika wakubwa

Mwaka 2018, Umoja wa Mataifa ulithibitisha kwamba watoto 1,106 waliuawa katika vita vya mzozo wa miaka tisa nchini Syria, hiyo ikiwa ni idadi ya juu zaidi ya watoto kuuawa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzuka kwa mzozo mwaka 2012 kwa mujibu wa UNICEF. Shirika hilo limesema idadi hiyo huenda ni ya juu zaidi huku mwenendeo huo ukishuhudiwa mwaka huu amapo kufikia sasa watoto 657 wameuwawa Syria.

UNICEF imesema kufikia mwezi Septemba mwaka huu, Umoja wa Mataifa umethibitisha matukio 1,792 ya ukiukaji wa haki za watoto mwaka huu pekee, ikiwemo mauaji, majeraha, uwandikishwaji kwa vikundi vilivyojihami na utekaji wa watoto na mashambulizi dhidi ya shule na vifaa vya afya.

Katika maeneo ya kaskazini-mashariki mwa Syria takriban watu 74,000 wakiwemo watoto 31,000 bado wamefurushwa na watu zaidi ya 15,000 wamekimbilia nchi jirani ya Iraq.

Kufikia sasa operesheni za UNICEF zimepokea asilimia 60 tu ya ombi la dola milioni 295 zinazohitajika kwa ajili ya operesheni za dharura nchini Syria.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter