Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Televisheni haifi ng’o!- ITU

Vijana wa kiume wakitizama soka kupitia televisheni Volta Redonda, Brazil.
Unsplash/Gustavo Ferreira
Vijana wa kiume wakitizama soka kupitia televisheni Volta Redonda, Brazil.

Televisheni haifi ng’o!- ITU

Masuala ya UM

Ikiwa leo ni siku ya televisheni duniani, shirika la mawasiliano la Umoja wa Mataifa, ITU limesema chombo hicho cha mawasiliano kitaendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika kuongeza uelewa wa masuala ya mambo miongoni mwa binadamu.

Katibu Mkuu wa ITU Houlin Zhao katika kauli yake ya siku hii anasema kuwa, “televisheni inaendelea kuwa na dhimu muhimu katika kuunganisha ulimwenguni wa kubadilishana taarifa ilihali ikipatia watumiaji chaneli nyingi zaidi za burudani.”

 Ameongeza kuwa ni kwa mantiki hiyo siku ya televisheni duniani inatoa fursa ya kuonesha kazi ya kipekee na ya mfano ya ITU ya kuzalisha kazi zinazozingatia viwango ambavyo vinachochea mwelekeo ujao wa utangazaji na huduma za intaneti ambazo zinasaidia kuwapatia watumiaji kote ulimwenguni uzoefu wa kipekee.

Kwa upande wake Mario Maniewicz, ambaye ni Mkurugenzi wa ofisi ya mawasiliano ya radio kwenye ITU amesema kuwa, “hivi sasa kuliko wakati wowote ule, televisheni inatoa taarifa, habari na burudani kwa watu popote pale walipo.”

 Kwa mantiki hiyo amesema,  “siku ya televisheni duniani inajikita sasa katika kazi ya ITU kwa zaidi ya miaka 70 ya kuendeleza mifumo ya viwango vipya vya utangazaji, na kuhakikisha vinaendana na teknolojia za kisasa zaidi zilizobuniwa ili matangazo ya televisheni yawe ya ubora zaidi na yapatikane kwa watu wote hata wale walio maeneo ya ndani zaidi.”

 Umoja wa Mataifa unakumbusha kuwa televisheni inaendelea kuwa chanzo kimoja kikubwa cha matumizi ya video na kwamba, “ingawa ukubwa na  umbo la skrini umebadilika na watu wanatumia na kuchapisha video kupitia majukwaa tofauti, bado idadi ya kaya zinazomiliki televisheni duniani inazidi kuongezeka.”

Halikadhalika umesema kuwa, mwingiliano kati ya teknolojia za kisasa za utangazaji na zile za zamani unajenga fursa ya kuongeza uelewa juu ya masuala muhimu yanayokabili jamii na dunia kwa sasa.

Je kuibuka kwa majukwaa mapya ya utangazaji ndio kifo cha televisheni ?

Swali hilo ameulizwa David Wood wa shirika la utangazaji la Muungano wa Ulaya, EBU ambaye amesema kuwa, “katu na kamwe! Kwa sababu televisheni inahusu maudhui na maudhui ni simulizi. Watu wamekuwa wakielezea simulizi kwa takribani miaka 500,000. Kwa hiyo televisheni haiendi popote. Bilas haka kutakuwepo na mbinu mpya, na za nyongeza za kuwasilisha maudhui kwa mtazamaji, lakini ile misingi ya wazo la kipindi cha televisheni itaendelea kuwa nasi hadi ukomo wa dunia na nina uhakika na hilo.

Na nini mustakabali wa televisheni?

Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa televisheni, Bwana Wood amesema bila shaka jambo muhimu zaidi linahusu ushirikiano kwenye teknolojia. “Kutumia mbinu za teknolojia za juu za mawasiliano ili kupata kipindi bora zaidi. Ingawa hivyo bado inasalia  kuwa unaelezea simulizi lakini mwishoni kuna ujumuishi mkubwa wa mtazamaji.”