Nasaidia wengine kama nilivyosaidiwa miaka 40 iliyopita-Mshindi wa tuzo ya Eleanor Roosevelt
Nasaidia wengine kama nilivyosaidiwa miaka 40 iliyopita-Mshindi wa tuzo ya Eleanor Roosevelt
Waswahili wanasema tenda wema nenda zako na pia wema hauozi. Mwezi huu tuzo ya haki za binadamu ya Eleanor Roosevelt imeenda kwa mtu ambaye miaka 40 iliyopita alikuwa mtoto maskini asiye na matumaini ya kuendelea kukanyaga darasani licha ya ufaulu wake kuwa mzuri.
Chris Mburu, akihojiwa na Priscilla Lecomte wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa anaeleza sifa zilizofanikisha kumpa tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka kwa watetezi bora wa haki za binadamu.
“Hiyo tuzo nimepewa kwasababu wameangalia ile kazi ambayo nimekuwa nikifanya katika Umoja wa Mataifa lakini kwa kazi yangu ya binafsi ya chama nilichoanzisha huko kwetu Kenya cha kusaidia watoto ili wasome kwasababu mimi nimesomeshwa na mtu ambaye alinionea huruma akanisomesha. Kwa hivyo baadaye nilianzisha chama ambacho kina jina la yule mwanamke kutoka Sweden ambaye alinisaidia.” Bwana Mburu Anafafanua.
Na kuhusu ni nini kilimfanya aishi kwa kutegemea misaada Anaeleleza, “mimi nilizaliwa katika familia maskini katika kijiji kinachoitwa Mitahato huko mkoa wa kati nchini Kenya. Na wakati ule elimu ilikuwa ya kulipia na familia yetu ikapata shida na mama yangu akatafuta msaada kwa wageni ambao walikuwa wanajihusisha na elimu ya watoto. Basi niliunganishwa na mwanamke mmoja kutoka Sweden ambaye anaitwa Hilde Back, sasa yule mama ndiye alinisomesha kuanzia shule ya msingi, ya sekondari na baadaye nikaenda chuo kikuu cha Kenya kusomea sheria na kisha chuo kikuu cha Harvard nchini Marekani. Na nimefurahi sana vile alivyonifanyia hata ndiyo maana nikasema chama changu kitakuwa n ajina lake yaani Hilde Back Education Fund na tunawasaidia watoto ambaao wako katika ile hali ambayo nilikwemo miaka arobaini iliyopita.”