Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa yaendelea kutilia mkazo utekelezaji wa haki za mtoto

Mtoto akiwa ameketi dawatini katika shule ya msingi mjini Doula, Cameroon  inayopatiwa ufadhili na UNICEF
© UNICEF/Tanya Bindra
Mtoto akiwa ameketi dawatini katika shule ya msingi mjini Doula, Cameroon inayopatiwa ufadhili na UNICEF

Mataifa yaendelea kutilia mkazo utekelezaji wa haki za mtoto

Haki za binadamu

Mataifa kadhaa hii leo Jumatano mjini Geneva Uswisi yameuuthibitishia ulimwengu ahadi yao ya kuboresha ulinzi wa haki za watoto wakati wa changamoto zinazotisha ikiwa ni pamoja na ubaguzi, vurugu, unyonyaji na umasikini.

Mataifa hayo yamethibitisha ahadi zao katika mkutano uliofanyika kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi wakati wa kuadhimisha miaka 30  tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto duniani. Mataifa hayo ni miongoni mwa mataifa 51 yaliyoitikia mwaliko wa kamati ya haki za mtoto ili kuiuhisha ahadi yao kwa kutoa ahadi mpya.

Bwana Luis Pedernera ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki za watoto amesema, "mkutano huo ndio makubaliano ya kwanza kutambua watoto kama wamiliki wa haki, wanastahili haki za binadamu ambazo ni za ulimwengu wote na haziwezi kuwa mjadala. Tangu kupitishwa kwake miaka 30 iliyopita, tumeshuhudia maboresho makubwa katika maisha ya watoto ulimwenguni kote. Tunasherehekea mafanikio haya. "

Mataifa ambayo ni sehemu ya mkutano huu yana jukumu la kuheshimu na kulinda haki za watoto wote wanaoishi chini ya mamlaka yao. Kila taifa duniani, isipokuwa Marekani, limeridhia mkataba huo na hivyo kuufanya mkataba huu kuwa mkataba wa haki za binadamu uliokubaliwa zaidi duniani.

Wakati Mkutano huo umesababisha kuimarika kwa kuheshimika zaidi kwa haki za watoto, Kamishna Mkuu wa UN wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet amesisitiza kwamba: "Katika ulimwengu unaokabiliwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira ya dijitali inayobadilika kwa kasi, mamilioni ya watoto bado wamebaki nyuma."