Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu mpya ya ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi ni jawabu la SDG14- FAO

Mfumo wa ufuatiliaji wa vyombo vya uvuvi majini na mfumo huu kutoka Sozopol Romania unawezesha kupata takwimu za uvuvi na mwelekeo wa meli za uvuvi
FAO/Claudia Amico
Mfumo wa ufuatiliaji wa vyombo vya uvuvi majini na mfumo huu kutoka Sozopol Romania unawezesha kupata takwimu za uvuvi na mwelekeo wa meli za uvuvi

Mbinu mpya ya ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi ni jawabu la SDG14- FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema atlasi mpya ya kufuatilia shughuli za uvuvi itasaidia kubaini shughuli za uvuvi kwenye maeneo mbalimbali duniani.

Atlasi hiyo mpya ya kimataifa ni  ya kwanza na ya aina yake na inachunguza fursa na changamoto za kutumia mfumo wa kubaini na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi, AIS.

Mfumo huo unasambaza taarifa kuhusu eneo meli iliko, utambulisho wake, mwelekeo pamoja na kasi na hivyo kuwezesha mamlaka kubaini meli hiyo inafanya shughuli gani mahali iliko.

FAO kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Roma, Italia, inasema kuwa hivi sasa idadi ya meli zinazotumia mfumo huo wa AIS inaongezeka kwa kati ya asilimia 10 hadi 30 kila mwaka na hivyo kuifanya teknolojia hiyo kuwa bora kila uchao.

Atlasi hiyo imezinduliwa kando mwa mkutano unaoendelea mjini Roma kuhusu uendelevu wa sekta ya uvuvi ambapo FAO imenukuliwa ikisema kuwa, “AIS inatupatia taarifa za kina za makumi ya maelfu ya meli za uvuvi na taarifa hizi za kina zina uwezo wa kutufahamisha makadirio ya shughuli za uvuvi na harakati hizo wakati zinaendelea.”

Hata hivyo FAO inasema kuwa teknolojia hii mpya ya ufuatiliaji inahitaji ukaguzi na tathmini ili wasimamizi wa sekta ya  uvuvi na watunga sera waweze kuelewa uthabiti na udhaifu wake.

Shirika hilo linasisitiza kuwa atlasi hiyo  yenye kurasa 400 inaweza kuthibitisha kuwa mbinu bora ya kuimarisha uvuvi endelevu na usimamizi sambamba na lengo namba 14 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Atlasi hiyo ni matokeo ya uchambuzi wa miaka 2 wa takwimu za kanda kwa kanda kwa kutumia ujuzi wa wataalamu 80 wa masuala ya uvuvi, takwimu za uvuvi za FAO na kanzi data nyingine za kisayansi.

Kwa mujibu wa atlasi hiyo, baadhi ya maeneo, AIS inaweza kupata takwimu sahihi zaidi za uvuvi mathalani kwenye eneo la kaskazini mwa bahari ya Atlantiki ambako inaweza kupata takwimu za meli yenye urefu wa mita 15 kwenda juu ilhali katika maeneo mengine hususan bahari ya Hindi, takwimu zinazoweza kupatikana ni finyu mno.

FAO inasema hiyo inatokana na uwepo wa meli ndogo za uvuvi.