Skip to main content

Nchi maskini zaidi elekezeni fedha za misaada kwenye mipango ya maendeleo- UN

Wavuvi wakipakua samaki aina ya jodari kwenye moja ya viwanda vya kuchakata samaki huko Abidjan, Côte d’Ivoire.
FAO/Sia Kambou
Wavuvi wakipakua samaki aina ya jodari kwenye moja ya viwanda vya kuchakata samaki huko Abidjan, Côte d’Ivoire.

Nchi maskini zaidi elekezeni fedha za misaada kwenye mipango ya maendeleo- UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Umoja wa Mataifa  umesema kuwa mataifa maskini zaidi duniani yanapaswa kuhakikisha kuwa fedha za misaada kutoka nje zinaelekezwa katika vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo.

Umoja wa Mataifa kupitia kamati yake ya maendeleo na biashara, UNCTAD imesema hayo katika ripoti  ya mwaka huu kuhusu mataifa hayo maskini zaidi duniani, LDCs.

Yaelezwa kuwa mataifa hayo ni 15 kati ya mataifa 20 yanayohitaji zaidi msaada na  hii kwa kiasi kikubwa inatokana na nchi hizo kukosa akiba ya fedha za ndani.

Katibu Mkuu wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema ili mataifa hayo yaweze kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kuepukana na utegemezi wa misaada, ni lazima yapatiwe msaada wa fedha kutoka nje.

Hata hivyo amesema ni lazima nchi hizo zimiliki ajenda yao ya maendeleo na kusimamia vyema uelekezaji wa fedha hizo za nje kwenye vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo na jamii ya kimataifa isaidie kufanikisha lengo hilo.

Ripoti hiyo inasema kuwa hivi sasa kuna muundo mpya wa utoaji wa  misaada ambao hata hivyo haujagusa maeneo ya maendeleo hasa kwenye miundombinu.

Mkuu wa kitengo cha LDCs katika UNCTAD Rolf Traeger anaesema kuwa uhusiano kati ya msaada wa fedha za kigeni na vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa unazidi kudhoofika akisema kuwa, “muundo wa msaada wa maendeleo wa kigeni, ODA unaegemea zaidi kwenye sekta za kijamii ambayo inapokea asilimia 45 ya msaada, ikilinganihshwa na miundombinu ya kiuchumi inayopokea asilimia 14 na ile ya uzalishaji asilimia 8.”

Kama hiyo haitoshi, ripoti inaonesha kuwa, mfumo wa sasa wa ufadhili umegubikwa na msururu wa kanuni na ulegezaji wa masharti unaompatia nafuu mkopaji lakini akijikuta analipa zaidi deni kwa hofu ya kuongeza deni la nje.

Kwa  mantiki hiyo UNCTAD inataka LDCs zichukue hatua kuweza kusimamia vyema fedha zake ambapo ripoti inasema kuwa, “kubadili mwelekeo huu ni lazima mataifa hayo yaimarishe usimamizi wa fedha zao za maendeleo . Hii inaweza kufanikiwa kwa kuanzisha au kuimarisha mfumo wa uratibu wa misaada, kama ambavyo inatekelezwa na mataifa hayo kama vile Rwanda na Jamhuri  ya watu wa Lao.”