Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msamaha wa rais wa Marekani kwa washukiwa wa uhalifu wa kivita unatoa taswira mbaya kwa wanajeshi kote ulimwenguni-OHCHR

Rais wa Marekani Donald Trump akihutubia mjadala wa wazi wa baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 25 Septemba, 2018
Picha UN/Cia Pak
Rais wa Marekani Donald Trump akihutubia mjadala wa wazi wa baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 25 Septemba, 2018

Msamaha wa rais wa Marekani kwa washukiwa wa uhalifu wa kivita unatoa taswira mbaya kwa wanajeshi kote ulimwenguni-OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imeelezea wasiwasi wake juu ya msamaha wa rais wa Marekani kwa wanajeshi watatu wanaoshukiwa kutekeleza uhalifu wa kivita.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa OHCHR, Rupert Colville amesema kesi za watatu hao zinajumuisha ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa unaodaiwa na uliothibitishwa ikiwemo kufuatilia kundi la raia na kuua kwa mtu aliyekamatwa wa kundi lililojihami.

Bwana Colville amesema sheria ya kibinadamu ya kimataifa inaweka masharti ya kuchunguza ukiukaji na kufungulia mashtaka uhalifu wa kivita na kwa kuchunguza madai hao na kudhihirisha na kumaliza mchakato wa kesi, mfumo wa sheria wa Marekani umekuwa ukizingatia majukumu haya chini ya sheria za kimataifa.

Amesema kuwa msamaha kamili katika kesi mbili, na amri inayoongoza kuendesha kesi ya tatu, vinaenda kinyume na mwongozo na misingi ya sheria ya kimataifa ambayo inahitaji uwajibishwaji kwa ukiukwaji huo na kwamba, "msamaha wa kusitisha kesi za jinai zinazosubiri kesi ya Meja Mathew Golsteyn unasikitisha, kwa sababu unakiuka mchakato wa kawaida wa mahakama."

OHCHR imesema, waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa wana haki ya kupata suluhisho na kwamba haki hii ni pamoja na upatikanaji sawa na madhubuti wa haki, haki ya ukweli, na kuona wahusika wakitumikia adhabu kulingana na uzito wa mwenendo wao, badala ya kuwaona wakiepuka uwajibishaji wowote.

Msemaji huyo wa OHCHR amesema, licha ya kwamba msamaha wa rais upo katika sheria za kimataifa, na unaweza kushughulikia kwa usawa masuala ya ukosefu wa haki, katika kesi zilizopo hakuna hali yoyote iliyotajwa kupendekeza chochote isipokuwa tu kuepuka mchakato sahihi wa sheria katika kesi hizo. 

Bwana Colville amehitimisha kwa kusema kuwa msamaha huu wa hivi karibuni unatoa ishara ya kutatanisha kwa vikosi vya jeshi kote ulimwenguni.