Zaidi ya watu milioni 2.4 wanahitaji msaada wa chakula ukanda wa Sahel ya Kati

19 Novemba 2019

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP leo limeonya kwamba dunia bado haijaelewa upana wa janga la kibinadamu linaloshuhidiwa ukanda wa Sahel ya kati ikijumuisha Burkina Faso, Mali na Niger.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa WFP Herve Verhoosel amesema watu milioni 2.4 wanahitaji msaada wa chakula haraka katika nchi hizo tatu. 

Ameongeza kwamba hali inayoshuhudiwa inachochewa na mapigano kati ya makundi yaliyojihami, ufurushwaji wa raia, njaa na umasikini uliotapakaa.

WFP imeonya kwamba iwapo hatua hazitachukuliwa sasa kukabiliana na njaa kizazi kizima kiko hatarini huko Bwana Verhoosel akisema  kwamba, “watu milioni 20 sasa wanaishi katika maeneo yaliyoathirika na mzozo katika ukanda na wanabeba mzigo wa janga linaloshuhudiwa wakati njaa na utapiamlo ukishuhudiwa. Tayari takriban watu 860,000 katika nchi tatu hizo za ukanda wa Sahel wamekimbia makazi yao na wamesalia wakimbizi ilhali zaidi ya 270,000 kati yao hao wamekimbilia nchi tatu jirani. Zaidi ya Elfu 26 wamekimbilia Burkina Faso, 187,140 wameenda Mali na elfu 56 nchini Niger.”

Ameongeza kuwa  mzozo umeathiri kilimo na uchumi vijijini na karibu mtoto mmoja kati ya watatu hayuko shule katika maeneo mengi yaliyoathirika na mzozo.

Shirika hilo limesema kuwa Burkina Faso iko katikati ya janga hilo wakati huu ambapo ongezeko la ukosefu wa usalama umesababisha shule kufungwa na wakulima kukimbia na kuacha mashamba yao katika nchi ambayo watu 4 kati ya 5 wanategemea kilimo. Aidha athari za mabadiliko ya tabianchi zinachochea uhasama kati ya wakulima na wafugaji ambao wanategemea raslimali kama maji na maeneo ya malisho.

Halikadhalika ongezeko la mapigano linaathiri ufikiaji wa familia zilizo na mahitaji.

Ingawa hivyo WFP tayari imeimarisha juhudi za msaada ambapo tayari imesaidia watu milioni 2.6 na chakula na mahitaji ya lishe.

Hata hivyo WFP inahitaji dola milioni 150 kwa ajili ya operesheni zake nchi hizo za Sahel chini ya programu zas asa ikiwemo shughuliza dharura na programu za kujengea jamii uwezo.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter