Kuondokana na nyuklia Mashariki ya Kati ni fursa kwa mataifa kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja-Guterres

18 Novemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kuanzisha eneo la Mashariki ya Kati bila silaha za nyuklia na silaha zingine za uharibifu wa watu, na kusema kuwa "majadiliano mazito" juu ya suala hilo itakuwa fursa kwa mataifa ya kanda kujihusisha katika "mazungumzo ya moja kwa moja juu ya mipango ambayo inaweza kushughulikia mahitaji yao ya usalama."

Akihutubia mkutano huo leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini  New York, Marekani, Guterres amesema maeneo yasiyokuwa na silaha za nyuklia yanamaliza kabisa uwezekano wa mzozo wa nyuklia katika eneo fulani na inaweza kutoa uhakikisho wa ziada kwa jamii ya kimataifa ya nia ya amani bila nyuklia katika nchi hizo katika eneo. 

Amesema maeneo kama hayo yametoa njia kwa mataifa kuchukua hatua na kufanya kazi kwa pamoja ili kuendeleza usalama wao wa kawaida wa eneo, na imewezesha vikundi vya mataifa kutoa michango huru katika kufafanua kanuni za ulimwengu na kuwezesha maendeleo katika mazungumzo ya jumla juu ya utokomezaji wa silaha.

Katibu Mkuu amesema umuhimu wa ukanda uliostawi wa Mashariki ya Kati unaenda mbali zaidi ya kanda hiyo. 

Ameelezea matumaini  yake kwamba mkutano huo utatumika kama "mwanzo wa mchakato unaojumuisha ambao mataifa yote ya ukanda huo yanaweza kushiriki." 

Ameongeza kuwa , kulingana na kanuni zilizokubaliwa ulimwenguni, ukanda wa Mashariki ya Kati ungehitajikuwa "matokeo ya hali maalum ya kanda na kuimarisha usalama wa mataifa yote."

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Sima Bahous, ambaye nchi yake ilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo, amesema washiriki wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja kuelekea hali ya ukanda wa Mashariki ya Kati bila silaha harubifu bila kukiuka haki ya mataifa binafsi ya matumizi salama ya nishati ya nyuklia.

"Leo, tunazindua njia ya miaka mingi ijayo ambayo imetoka ndani ya ukanda wa Mashariki ya Kati, na ili sisi katika miaka ijayo kufikia lengo la mwisho la kufikia makubaliano ya mkataba wa kisheria, ni muhimu kwamba ujumuishaji, uwajibikaji, na umiliki wa pamoja unapaswa kudhibiti mchakato huu," amesema Balozi Bahaous.

 Naye mwakilishi wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa amesema ushiriki wa mataifa yote kasoro taifa moja, inathibitisha umuhimu ulioyapa mataifa yaliyowakilishwa, pamoja na taifa la Palestina, kutekeleza ahadi na majukumu yao katika kuufanya ukanda huu na ulimwengu kuwa mahali salama na huru na aina hizo za silaha.

Mwakilishi wa kudumu wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Majid Ravanchi amesema kuwa kufanikiwa kwa mkutano huo hakika kutachangia amani na usalama wa kimataifa kupitia kukomesha aina zote tatu za silaha za maangamizi, ambazo ni silaha za nyuklia, kemikali, na kibayolojia. Walakini, alisisitiza kwamba ili kufanikisha azma hii, nchi zinazoshiriki kikanda pamoja na nchi zenye silaha za nyuklia zinapaswa kuamua kuingia katika mazungumzo yenye maana na kukubaliana na kuheshimu majukumu maalum.

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud