Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwapa uongozi wanawake Rumbeki ni kuipa jamii uongozi-UNMISS 

Wanawake viongozi washerehekea baada ya kufungwa kwa warsha ya uwiano na kutatua mizozo JUba nchini Sudan Kuisni.
UNMISS
Wanawake viongozi washerehekea baada ya kufungwa kwa warsha ya uwiano na kutatua mizozo JUba nchini Sudan Kuisni.

Kuwapa uongozi wanawake Rumbeki ni kuipa jamii uongozi-UNMISS 

Amani na Usalama

Jamii ya Rumbek nchini Sudan kusini imepitia changamoto nyingi tangu kuzuka kwa machafuko lakini sasa mambo yanaanza kubadili kuanzia nyumbani, katika meza ya maamuzi na hata katika mchakato wa kuleta amani.

Katika jimbo la Western Lake mjini Rumbek wanawake wamekusanyika kusherehekea uteuzi wa wenzao wawili kushika nyadhifa na majukumu muhimu katika jamii.

Lengo lao ni kutoa asante kwa uongozi wa wanaume wa eneo hilo kwa kubadili fikra na kuwezesha uteuzi huo kutokea. Wanaweka njiwa ambaye ni ishara ya kimataifa ya amani mabegani kwa naibu gavana ikiwa ni ishara ya shukran zao.

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS unasema uteuzi huo wa kihistoria ni wa mwanamke wa kwanza kabisa kuwahi kuteuliwa katika mahakama ya kijadi, Ayor Achor Kuer anayetarajia kuleta mabadiliko,“Sintoogopa kuwasilisha masuala ya wanawake hata kama mimi ni mwanamke pekee miongoni mwa wanaume. Naamini hatua hii ya jimbo la Western Lake itaigwa kila mahali ili wanawake waweze kuteuliwa kama wajumbe wa mahakama za kijadi. Watu wa jimbo la Lake wanaheshimu sheria na kama unavyojua sheria inawafanya watu kuishi kwa amani. Na pia sitaki kuwa ndiye mwanamke pekee ninayewakilisha wanawake. Natoa wito kwa serikali na mamlaka ya kijamii kuteua wanawake zaidi kuendesha mfumo wa haki katika ngazi mbalimbali.”

Na mwanamke wa pili aliyeteuliwa ni Ayen Majok Deng ambaye ameaapishwa hivi karibuni kuwa waziri wa elimu katika serikali ya kikanda,“Sio tu kwamba mimi ni waziri mwanamke lakini pia ni waziri kijana. Hivyo nafasi yangu inamaanisha kwamba nitawakilisha wote wanawake na vijana. Inamaana kubwa sana kwa wanawake na wasichana wa Western Lake hususan wasichana wadogo. Itawachagiza kwenda shule na kusoma kwa bidi hivyo mimi ni kama mfano kwa wanawake wa jimbo la Western Lake.”

Idadi kubwa ya wanawake Sudan Kusini wamesahaulika, kutengwa, na wachache sana wanaosoma hali ambayo inazima ndoto zao za kuweza kushika nafasi zozote za madaraka.

Caroline Opok ni mkuu wa kitengo cha misaada, ujumuishi na ulinzi katika ofisi ya UNMIS mjini Rumbek,“Hivyo mtazamo ni jinsi gani wanawake, jinsi gani serikali na kila mtu anayehusika atasaidia wanawake kujiwezesha wenyewe, kwa sababu uwezeshaji ndio changamoto. Ni elimu gani Ni shughuli gani za kiuchumi na jinsi gani vimewekwa ili kusaidiana na kuinuana?”.

Matumaini ya UNMISS ni kwamba wanawake hao wakiwezeshwa wataiwezesha jamii na kuchagiza amani.