Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaafrika Mashariki tuoane ili tusukume gurudumu la jumuiya- Jaji Lenaola

Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Jaji Isaac Lenaola.
UN News
Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Jaji Isaac Lenaola.

Wanaafrika Mashariki tuoane ili tusukume gurudumu la jumuiya- Jaji Lenaola

Masuala ya UM

Kuaminiana miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, pamoja na utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi ni muhimu ili mataifa hayo yaweze kufikia muungaon wa kisiasa. Priscilla Lecomte na taarifa kamili.

Hiyo ni kauli ya Naibu Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Isaac Lenaola aliyoitoa wakati akihojiana nami hivi karibuni huko Asmara nchini Eritrea kandoni mwa mkutano wa kila mwaka wa Tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa nchi za Afrika UNECA.

Jaji Lenaola alitoa kauli hiyo akizingatia kuwa muungaon wa kisiasa utafungua fursa zaidi za maendeleo kwenye ukanda huo, akisema kuwa, “tangu Jumuiya iundwe mwaka 2000, ni mwaka 2017 ndiyo tumepata sheria ambayo inasema tuanze mazungumzo juu ya ushirikiano wa kisiasa. Na muundo wa kisiasa ni jukumu kubwa sana. Kwa hiyo kama tumechukua miaka 17 kuanza mazungumzo, je kuiunda, itawezekana miaka 30 au 40 ijayo? Sioni mimi.”

Kwa mantiki hiyo, akanieleza kuwa ni lazima kubadilisha mifumo yetu ya kisiasa, lakini  pia, kuhakikisha wananchi wenyewe wanahamasishwa akisema, “ sisi wenyewe waafrika wa mashariki, tuoane katika jumuiya, tusafiri katika jumuiya, tutalii katika jumuiya, tuwapeleke watoto wetu shule katika nchi jirani. Tukifanya hivyo, watu wetu watakuwa wale wanaosukuma gurudumu la kuiunda jumuiya.”

Kuhusu Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jaji Lenaola ameeleza kwamba tangu kuundwa kwake mwaka 2006, imeshasikiliza takribani kesi 3,000 kutoka kwa wananchi wa nchi zote za ukanda huo.

Amekumbusha kuwa jukumu kubwa la mahakama hiyo ya haki ya EAC ni kuhakikisha kwamba mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unafuatiliwa na kulinda utengamano katika ukanda huo, kila mwananchi akiwa na haki ya kupeleka kesi yake mahakamani.

Kuhusu lugha, amesema itakuwa vyema kukubali kwamba Kiswahili kiwe lugha rasmi ya jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati sasa badi ni kiingereza pekee.