Miradi miwili ya maji Kyaka na Kyangwali yaondoa adha kwa wakimbizi na wenyeji

12 Novemba 2019

Nchini Uganda, wakimbizi wanaoishi kwenye makazi ya Kyaka na Kyangwali pamoja na wenyeji wao wameanza kunufaika na miradi miwili ya maji iliyojengwa na shirika la uhamiaji duniani, IOM kwa msaada wa fedha kutoka Muungano wa Ulaya, EU.

Mradi huo uliogharimu Euro milioni 2, umewezesha ujenzi wa mifumo miwili ya maji ya bomba ikiwa ni sehemu ya mradi wa mwaka mmoja uliolenga kuimarisha miundombinu ya maji na huduma za kujisafi kwa wakimbizi na wenyeji wao nchini Uganda.

IOM ilichukua hatua hiyo kufuatia ongezeko la wimbi la wakimbizi nchini Uganda lililosababisha mvutano wa matumizi ya rasilimali hiyo kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyaka na Kyangwali, hali iliyosababisha pia milipuko ya magonjwa.

Katika ujenzi wa mradi huo, huko Kyangwali, IOM ilitandaza kilometa 25 za mtandao wa mabomba ya maji pamoja na kujenga tanki la ujazo wa lita 100,000 za maji likiwa na mabomba 30.

Huko Kayka, mfumo mpya wa maji unaweza kusukuma lita 42,000 za maji kwa saa na unalenga kuhudumia zaidi ya watu efu 21.

Mkuu wa IOM Uganda ambaye amemaliza muda wake, Ali Abdi, amepongeza mchango wa wahisaji akisema mifumo hiyo ya maji inaonesha usaidizi wa dhati wa Muungano wa Ulaya na fuko la usaidizi la dharura la Umoja wa Mataifa, CERF katika kulinda na kuimarisha maisha ya wakimbizi kwenye makazi nchini Uganda. 

Akizungumzia kuhusu mifumo hiyo miwili  yamaji, Kamishna wa misaada wa kibinadamu EU, Christos Stylianides amesema msaada huo utapunguza utegemezi wa mgao wa maji kupitia malori, jambo ambalo amesema si endelevu.

Halikadhalika amesema uwepo wa huduma hiyo ya maji siyo tu inasaidia kuhakikisha kuwa jamii na wakimbizi wanatapa maji safi na salama bali pia itaepusha hatari ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana ambao hulazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter