Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kusomea mtoto kitabu kabla ya kulala husaidia mtoto kulala muda mrefu - Ripoti, WHO

Sanaa
Jorge Mario Álvarez Arango
Sanaa

Kusomea mtoto kitabu kabla ya kulala husaidia mtoto kulala muda mrefu - Ripoti, WHO

Afya

Kujihusisha na sanaa kunaweza kuwa na faida za afya ya akili na kimwili, imesema ripoti mpya ya shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Ulaya iliyojumuisha utafiti kutoka machapisho 900 kote ulimwenguni ikiwa ni utafiti wa undani kabisa kuhusu sanaa na afya.

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya, Dkt. Piroska Östlin amesema, “kuleta sanaa katika maisha ya watu kupitia dansi, kuimba na kutembelea majumba ya kumbukumbu na matumbuizo kunatoa fursa ya jinsi ya kuimarisha afya ya mwili na akili.”

Dkt. Östlin amesema, “mifano iliyoorodheshwa katika ripoti hiyo ya WHO inaonyesha mbinu ambazo sanaa inaweza kukabiliana na changamoto nyingi za kiafya ikiwemo kisukari, utipwatipwa na afya ya akili.”

Ripoti imeonesha kuwa afya na uzima wa mwili vinaangaziwa kwa mapana zaidi na kwa muktadha wa jamii na vinatoa suluhu ambazo mifumo ya kitabibu kwa sasa imeshindwa kuangazia kikamilifu.

Kwa mujibu wa ripoti kuanzia kuzaliwa hadi kifo, sanaa inaweza kuwa na mchango chanya kwa afya kwa mfano, watoto wachanga ambao wazazi wao wanawasomea vitabu kabla ya kwenda kulala wanakuwa na usingizi wa muda mrefu na umakini shuleni. 

Aidha miongoni mwa barubaru wanaoishi mijini, elimu kupitia michezo ya kuigiza kati ya watu wa rika moja inaweza kusaidia katika kufanya mamuzi muhimu, kuimarisha uzima na kupunguza uwezekano wa ukatili. Katika maisha ya baadaye, muziki unaweza kusaidia watu wanaougua ugonjwa wa kusau ambapo kuima kumethibitishwa kuimarisha umakinifu, kumbukumbu na utendaji.

Kwa sasa nchi nyingi zinaangalia namna ambavyo wanaweza kujumuisha sanaa katika mfumo wa matibabu ambapo madakatari wanapendekeza wagonjwa kujihusisha na shughuli za sanaa.

Ripoti imeainisha sera kwa ajili ya watunga será katika sekta ya afya na kwingineko kwa mfano, kuhakikisha uwepo na ufikiaji wa programu za sanaa kwa ajili ya afya katika jamii na zinazounga mkono sana na mashirika ya kitamaduni katika kuhakikisha afya na uzima wa mwili ni sehemu ya kazi zao, kuimairisha uelewa wa umma kuhusu faida ya kushiriki sanaa ikiwemo kujumuisha sanaa katika mafunzo ya wahudumu wa afya na kuwekeza zaidi katika utafiti hususan katika kuimarisha programu za afya na kuchunguza utekelezaji wake.