Chonde chonde wabolivia kaeni mbali na machafuko:Guterres

11 Novemba 2019

Kufuatia hali ya wasiwasi inayoendelea nchini Bolivia baada ya kujiuzulku kwa rais wa nchini hiyo Evo Morales mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka raia wote wa nchi hiyo kujizuia na machafuko na mamlaka kuhakikisha ulinzi na usalama  kwa raia wote, maafisa wa serikali na raia wa kigeni.

Antonio Guterres katika tarifa iliyotolewa leo kupitia kwa msemaji wake ametoa wito wa kuheshimu taasisi za kiserikali pamoja na kutokiuka sheria za masuala ya kiplomasia.

Katibu Mkuu amesema anaendelea kuwa na hofu kubwa kuhusu hali nchini Bolivia na amezitaka pande zote kupunguza mvutano, kuzingatia sheria za kimataifa na kuheshimu misingi ya haki za binadamu.

Pia amewaomba wadau wote kuhakikisha wanafikia suluhu ya amani ya mgogoro wa sasa na kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa wa kuaminika, huru na wa wazi.

Rais Morales amejiuzulu baada ya wiki tatu za mvutano mkubwa wa kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 20 ambao ulimtangaza yeye kuwa mshindi na kumpa fursa ya kuongoza serikali kwa awamu ya nne.

Kupitia hotuba yake kwa njia ya televisheni rais Morales aliyekuwa madarakani kwa miaka 14 amesema amejiuzulu kwa ajili ya ‘maslahi ya taifa” lakini akaongeza kwamba “nguvu za giza zimesambaratisha demokrasia ya nchi hiyo”

Upinzani walimtaka Rais huyo kujiuzulu kufuatia kutangazwa kwa uchaguzi mwingine nchini humo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud