9 Novemba 2019

Ndani ya misitu minene kaskazini mwa Jamhuri ya Congo, kunapatikana kundi la wanawake waliojitolea kusaidia jamii zilizoko maeneo ya ndani zaidi kutokomeza utapiamlo.

Akiwa kijijini Mbanza, Véronica Etima alikuwa anaonekana kuwa na wasiwasi. Aliweza kuona kuna kitu kibaya kinakumba watoto kwenye jamii yake. Walikuwa wakionesha baadhi ya dalili alizoziona kwa mpwa wake kabla ya kufariki dunia.

“Mwanzoni, hatufahamu kilichotokea. Lakini niliweza kuona kuwa watoto wengi katika jamii yetu walikuwa wakionesha dalili zile zile. Kwa hivyo, niliamua kujifunza. Ndipo tuligundua kuwa kifo chake kilisababishwa na utapiamlo,” anasema Véronica akizungumzia Mbandza, kijiji kidogo cha watu wa jamii ya asili katika misitu ya eneo la kaskazini mwa Jamhuri ya Congo.

UNICEF/UNI212587/Tremeau
Véronique Etima, mwanachama wa kikundi cha wanawake kinachoelimisha dhidi ya utapiamlo.

 Unyafuzi, au utapiamlo uliokithiri, unaathiri takriban theluthi moja ya watoto kwenye eneo la Likouala. Lakini 'Mama Véronica', kama anavyojulikana kijijini, alikuwa amedhamiria kuelewa kile kinachotokea na kubadili mustakabali  wa watoto wa Mbandza. Alichojifunza kuhusu lishe sio tu kusaidia kutunza afya ya mtoto wake, lakini pia imemwezesha kutoa ushauri kwa familia nyingine, ushauri ambao pia unaweza kuokoa maisha.

 

UNICEF/UNI212596/Tremeau
Kijiji cha Mbandza, moja ya maeneo yaliyoko ndani zaidi huko Jamhuri ya Congo.

 Kijiji cha Mbandza, kimezungukwa na misitu minene, takriban kilomita 1,300 kaskazini mwa Brazaville, mji wa mkuu wa Jamhuri ya Congo. Ni safari ya zaidi ya siku mbili kutoka mji huo na kupitia mito na barabara zenye matuta, moja ya maeneo ya Jamhuri ya Congo, yaliyo ndani zaidi.

UNICEF/UNI212591/Tremeau
Mama Veronique akiwa na mwanae mwenye umri wa miezi 13.

Mama Véronica akiwa amembeba Isidore, ambaye ni mwanae mwenye umri wa miezi 13,amehudhuria  huduma ya kuchunguza iwapo mtoto huyo ana utapiamlo. Baada ya kumpoteza mpwa wake, aliazimia kufanya kila kilichohitajika ili kuhakikisha kuwa wazazi katika jamii yake wasipitie ule uchungu wa kumpoteza mtoto kwa utapiamlo.

Anasema alipata ujumbe kuhusu Chama cha mapambano dhidi ya utapiamlo, shirika la kiraia lililoanzishwa mnamo mwaka 2007, na kwa haraka kuwa mshiriki wa kikundi cha shirika hilo cha wanawake wa kuangazia mwanga kwenye jamii au Femmes Lumières. Kikundi hiki kilipatiwa mafunzo ya  kusaidia katika mapambano dhidi ya utapiamlo miongoni mwa watoto.

UNICEF/UNI212596/Tremeau
Mama Veronique akiwa anapita msituni kusaka chakula cha familia yake.

Jamii asilia nchini Jamhuri ya Congo,  hutegemea kula chochote wanachoweza kupata kutokana na uvuvim uwindaji au chochote kile msituni na hivyo kuwaacha wengi wao na wigo mdogo wa lishe bora. Hata hivyo, Mama Véronica anasema kuwa chakula kingi anachotayarishia familia yake ni mazao ambayo amevuna, kwenye mashamba yaliyo misituni.

UNICEF/UNI212593/Tremeau
Mama Veronique akivuna mazao aliyopanda.

Mama Véronica anavuna baadhi ya mazao ambayo amepanda. Mazao ya chakula yanayolimwa hivi sasa, au ambayo yanapatikana kijijini kama vile mchicha wa pori, mihogo, tikiti, njugu karanga, soya na viazi vikuu, hutumika kujazia viambato na vyakula vingine vilivyokusanywa kwa njia za kijadi za uwindaji au uvuvi.

 

© UNICEF/UNI212586/Tremeau
Mama Veronique akiandaa mlo wa familia yake.

Vyakula vya kijadi vinamwezesha Maman Véronique na wengine kuandalia familia zao milo iliyo kamilifu.

“Nimegundua kuwa kuna aina tofauti ya vyakula ambavyo, vinapochanganywa, vinaweza kusaidia kulinda na kuwapatia watoto nguvui,” anasema Maman Véronique.

UNICEF/UNI212594/Tremeau
Mama Veronique akipata mlo na familia yake.

 Mama Véronica sasa mlo tayari, yeye na mwanae wa kiume pamoja na watoto wawili anaowalea wanapata mlo pamoja. Ana furaha kwamba mwanae ni mzima na mwenye afya, lakini pia anafurahi kuwa ameweza kusaidia watoto wengine kwenye jamii.

UNICEF/UNI212592/Tremeau
Mama Veronique akiwa anapika mlo kufundisha wengine.

Mama Véronica sasa anaongoza madarasa ya upishi bora  akiwafundisha wazazi jinsi ya kuandaa milo yenye afya na ile inayopatikana sokoni. Viwango vya utapiamlo ni vikubwa sana miongoni mwa watu wa jamii ya asili wanaoishi katika mazingira magumu katika eneo hilo la Mbandza, ambapo jamii hazipati hata huduma za msingi za afya na taarifa kuhusu lishe.

UNICEF/UNI212590/Tremeau
Mama Veronique na wenzake hutembelea pia vijiji vya jirani kusambaza elimu.

Wawakilishi wa kikundi cha wanawake wanaoelimisha dhidi ya utapiamlo pia huongoza shughuli za kuhamasisha kuhusu athari za utapiamlo katika mji wa karibu wa Bétou. Mama Véronica, akishikilia bango, anasema kuwa amefahamu umuhimu wake unaohitajika, na sasa pia husaidia kuongoza baadhi ya madarasa akisema kuwa, “nilijifunza kuwa kunyonyesha tu hadi umri wa miezi sita ni jambo bora sana ambalo mama anaweza kumfanyia mtoto wake. Pia nilijifunza jinsi ambavyo usafi na usafi wa mazingira ni muhimu katika kukabiliana na utapiamlo.”

UNICEF/UNI212588/Tremeau
Elimu yao husambaza pia vijiji vya jirani.

Wawakilishi wa kikundi cha wanawake wanaoelimisha kuhusu utapiamlo, wanaonyesha wazi jinsi ya kuandaa mlo wenye afya. Kikundi chenyewe hufanya shughuli mbali mbali, pamoja na kueneza ujumbe juu ya usafi na usafi wa mazingira, kuendesha huduma za afya za nyumba kwa nyumba, pamoja na chanjo, karibu na idadi ya watu waliotengwa. Shirika lenyewe pia linatoa hatua za kuimarisha kilimo ili kusaidia jamii kubadilisha uzalishaji wa chakula na kuleta mapato, pamoja na kutumia kinu kinachotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kusindika soya.

UNICEF/UNI212595/Tremeau
Maonyesho ya mapishi si tu kwa watu wazima hata watoto nao wamenufaika.

Maonyesho ya kupika hayakusudiwi tu watu wazima, bali watoto pia huchangia wakisaidiwa na wawakilishi wa kikundi cha wanawake wanaoelimisha dhidi ya utapiamlo.

 “Kidogo kidogo, mambo yanabadilika,” anasema Mama Véronica, akisisitiza kwamba hatua hizi zinasaidia afya ya watoto katika jamii akiongeza kuwa, “tunaona idadi ya watoto wenye dalili za utapiamlo ikipungua. Bado kuna kazi ya kufanya, lakini wanajamii wenzangu wanaelewa na wamekubali kuwa tunahitaji kubadilisha mazoea kwa sababu ya watoto wetu ili wawe na mustakabali bora.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud