Utekelezaji wa SDGs unakwenda mrama- Guterres

7 Novemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wikii ameandika tahariri iliyochapishwa kwenye gazeti la Financial Times na kutoa wito kwa viongozi wa kibiashara duniani kutumia ushawishi wao mkubwa katika kusongesha ukuaji jumuishi na fursa za kunufaisha wakazi wote wa sayari ya dunia.

Katibu Mkuu amesema maendeleo katika kufanikisha maendeleo endelevu yanasuasua kwa kiasi kikubwa, njaa ikiongezeka, nusu ya wakazi wa dunia hawana elimu na huduma za afya, wanawake wakizidi kukumbwa na ubaguzi.

 “Kwa kweli ni maadili mema na biashara bora kuwekeza katika maendeleo endelevu na yenye usawa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “uongozi wa kibiashara unaweza kuleta tofauti kubwa katika mustakabali wa amani, utulivu na ustawi kwenye sayari iliyo bora.”

Amezungumzia mwenendo wa maandamano hivi karibuni duniani kote ambako watu wameingia mitaani kupinga kupanda kwa gharama za maisha sambamba na ukosefu wa haki.

“Wanahisi kuwa uchumi hauna maslahi kwao, na katika maeneo mengine wako sahihi. Kujikita tu katika ukuaji uchumi, bila kujali gharama yake halisi na matokeo yake, kunasababisha janga la tabianchi, watu kupoteza imani na taasisi na kukosa imani na mustakbali,” amesema Katibu Mkuu.

Kwake yeye, Bwana Guterres anaamini kuwa sekta binafsi ni muhimu katika kutatua matatizo hayo, na kwamba sekta ya biashara imekuwa ikifanya kazi na Umoja wa Mataifa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs tangu yalipopitishwa mwaka 2015.

Malengo hayo 17 yanalenga kushughulikia matatizo kama vile, njaa, ukosefu wa usawa, janga la tabianachi, amani na haki na yanataka kuwa angalau matatizo hayo yashughulikiwa kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Utekelezaji wa SDGs unakwenda mrama

Hata hivyo Katibu Mkuu anahofia kuwa utekelezaji unakwenda mrama kwa kuwa tangu malengo hayo yapitishwe, licha ya kupungua kwa kiwango cha uhohehahe na vifo vya watoto wachanga.

“Ukosefu wa fedha ndio sababu kuu. Upelekaji wa fedha za umma kwenye maeneo hayo yautoshi na Umoja wa Mataifa  unashirikiana na sekta ya fedha kuziba pengo,” amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa sekta ya biashara inahitaji sera za muda mrefu za uwekezaji ambao zitasaidia si tu wamiliki wa hisa bali pia jamii akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa na sekta binafsi wanashirikiana kusaka njia mpya za kuwekeza katika ukuaji endelevu na maendeleo.

Mwezi uliopita, viongozi 30 wa kampuni za kimataifa walikutana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kuzindua ushirika wa wawekezaji wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu na tayari ubia huo unaunga mkono miradi ya nishati salama barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Shinikizeni mabadiliko ya sera

Katibu Mkuu ametoa wito kwa sekta ya biashara kusonga zaidi ya kuwekeza bali pia kushinikiza mabadiliok ya sera akisema kuwa walaji tayari wanaweka shinikizo.

“Tunataka viongozi wa biashara watumie ushawishi wao mkubwa kushinikiza ukuaji uchumi jumuishi na fursa”  akisema kuwa “hakuna biashara hata moja itakayoweza kupuuza harakati hiyo na kwamba hakuna lengo la kimataifa ambalo halitanufaika na uwekezaji wa sekta ya biashara.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Viongozi wakuu 30 kutoka sekta za biashara kujiunga na UN kufanikisha maendeleo endelevu

Umoja wa Mataifa umetangaza leo kuwa viongozi 30 wenye ushawishi kutoka sekta za biashara watashirikiana katika kipindi cha miaka miwili ijayo katika jaribio la kufungulia matrilioni ya dola kutoka sekta ya kibinafsi kufadhili maendeleo endelevu.