Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hukumu dhidi ya mshukiwa wa ubakaji nchini Mauritania yakaribishwa: OHCHR

Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR
UN Photo.
Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR

Hukumu dhidi ya mshukiwa wa ubakaji nchini Mauritania yakaribishwa: OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR,  imekaribisha hukumu ya kifungo cha miaka 5 gerezani iliyotolewa nchini Mauritania dhidi ya mwanaume mwenye umri wa miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka msichana  mwenye umri wa miaka 15 huku ikisema kuwa ni hatua chanya katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na ukatili wa kijinsia. 

Akizungmuza na wandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi, Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, amesema wamekaribisha hukumu hiyo iliyotolewa Kusini mwa Mauritania kwani  kwa muda mrefu karibu washukiwa wote wa ukatili wa kijinsia hasa ubakaji hawaadhibiwi nchini humo.

Hivyo ametolea wito serikali ya Mauritania kuhakikisha kwamba mtoto aliyebakwa analipwa fidia kwa kuzingatia umri wake na jinsia.

Bwana Colville amesema rasimu ya sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia imepuuzwa mara mbili ilipofikishwa kwenye Bunge la taifa hilo lisilokuwa na sheria yoyote dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Halikadhalika Bwana Colvile amechukua nafasi hii pia kulihimiza bunge la Mauritania kurejesha upya na kujadili mswada wa sharia hiyo na kufanya haraka iwezekanavyo kupitisha sheria inayoendana na vigezo vya kimataifa vya haki za binadamu.

Pia ameitolea wito serikali ya kutekeleza sheria hiyo mara baada ya kupitishwa na kuweka mkakati imara wa kupambana na tatizo hilo lililokita mizizi na kuathiri karibu taifa zima la Mauritania.

Katika muktadha huo Bwana Colville ametangaza kuwa maadhimisho ya mwaka huu ya siku 16 za harakati za kupinga ukatili wa kijinsia yatajikita katika suala la ubakaji.