Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa msaada waongeza kiwewe kwa wakimbizi na wahamiaji watoto waliotimiza umri wa utu uzima Italia- Ripoti

Omar mwenye umri wa miaka 17, (kulia kabisa mstari wa pili) na wavulana wengine ambao wamefika Italia bila wazazi, wakiwa kwenye jengo moja la kanisa lililotelekezwa huko Sicily, Italia. Wengi wao walifikishwa kijiji hiki kidogo bila ridhaa yao.
© UNICEF/Stefano De Luigi
Omar mwenye umri wa miaka 17, (kulia kabisa mstari wa pili) na wavulana wengine ambao wamefika Italia bila wazazi, wakiwa kwenye jengo moja la kanisa lililotelekezwa huko Sicily, Italia. Wengi wao walifikishwa kijiji hiki kidogo bila ridhaa yao.

Ukosefu wa msaada waongeza kiwewe kwa wakimbizi na wahamiaji watoto waliotimiza umri wa utu uzima Italia- Ripoti

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani wakimbizi na wahamiaji watoto 60,000 waliowasili  nchini Italia bila wazazi ama walezi kati yam waka 2014 na 2018 ambao sasa wametimiza umri wa miaka 18 wanahitaji msaada endelevu ili waweze kumudu kipindi cha mpito cha kuwa watu wazima.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF, la wakimbizi, UNHCR na lile la wahamiaji.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina: Wakiwa njiapanda: Watoto wasio na wazazi au waliotenganishwa na wazazi katika mpito wa utu uzima italia, inaangazia kile ilichoita vipindi vitatu vya mpito ambavyo watoto hao wanapitia wanapotimiza umri wa miaka 18.

Vipindi hivyo ni kutoka ubarubaru kwenda utu uzima, kuishi nchi moja hadi nyingine na kupitia machungu ya hisia na kiwewe wakati wanaondoka nyumbani na wakati wa safari hatari za kuelekea Ulaya.

Wahamiaji wawili vijana kutoka Gambia wakiangalia ramani baada ya kuvuka Italia mwaka 2016.(Maktaba)
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Wahamiaji wawili vijana kutoka Gambia wakiangalia ramani baada ya kuvuka Italia mwaka 2016.(Maktaba)

Anna Riatti ambaye ni mratibu mkazi wa UNICEF Italia amesema, “tofauti kati ya mkimbizi au mhamiaji mwenye umri wa miaka 17 aliyekimbia mzozo au ghasia na ya mwenye umri wa miaka 18 aliyekumbwa na kiwewe ni ndogo sana na uwezekano wa kupoteza msaada kwa makumi ya maelfu ya vijana kutokana na utofauti wa kiumri, utawaweka katika hatari ya kutengwa kijamii, ghasia, kunyanyaswa na hata mustakabali wa mashaka.”

Kwa upande wake Roland Schilling ambaye ni mwakilishi wa UNHCR kusini mwa Ulaya amesema kutambua tofauti kati ya mtoto na mtu mzima na kutambua kuwa watu wanaobalehe wana mahitaji muhimu ndio msingi wa utafiti wa ripoti hii.

Amesema kwa kuwa na uelewa dhahiri wa vigezo vinavyohamasisha au kukwamisha mpito chanya kutoka kuwa mkimbizi mtoto hadi kuwa mtu mzima anayejitegemea na mwenye mnepo kutasaidia mataifa kuimarisha juhudi zao za kulinda siyo tu wakimbizi watoto bali pia kipindi bora zaidi cha mpito kuelekea utu uzimani.

Miongoni mwa vigezo vinavyokwamisha mpito bora kutoka mkimbizi mtoto hadi mtu mzima ni pamoja na mchakato mgumu au unaosuasua wa kupata nyaraka halali, ubaguzi, mkwamo katika kupata elimu na mafunzo ya kazi, kukabiliana na kiwewe na pia hatari ya ukatili hususan wasichana.

Kwa mantiki hiyo ripoti inataka katika vipindi hivyo vigumu vya mpito, watoto wakimbizi na wahamiaji wanahitaji msaada kama vile uhusiano chanya na watu wa rika lao pamoja na walezi, elimu, mafunzo ya stadi, fursa za ajira, na makazi salama.

Mapendekezo kwa mamlaka za Italia

Ripoti hiyo inataka serikali ya Italia ipitishe mkakati wa kisekta wa kitaifa ili kuongeza ujumuishaji wa kijamii kwa wakimbizi vijana ambao wametimiza umri wa miaka 18 pamoja na mpango wa kitaifa dhidi ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi.

Halikadhalika kuhakikisha utekelezaji wa kina wa sheria namba 47/2017 kuhusu ulinzi wa watoto walio peke yao ambao wanasaka hifadhi au UASC.

Nchini Italia, mvulana, amesimama nje katika mtaa duni katika mji wa Turin, eneo la Piedmont.
UNICEF/UNI173328/Pirozzi
Nchini Italia, mvulana, amesimama nje katika mtaa duni katika mji wa Turin, eneo la Piedmont.

Kamisheni ya Ulaya nayo ina jukumu

Mashirika hayo matatu ya Umoja wa Mataifa pia yanataka Kamisheni ya Muungano wa Ulaya ichukue hatua kama vile kufanikisha ushirikiano wa dhati baina ya nchi wanachama katika kutathmni maslahi bora zaidi ya kila mtoto na kutekeleza kanuni za kuwaunganisha na familia zao.

Ianzishe pia mfumo wa kukusanya takwimu na taarifa sahihi kuhusu hali ya watoto wa sasa na wa zamani ambao hawakuwa wameambatana na wazazi au walezi na pia kubainisha rasilimali chini ya mfuko ujao wa Kamisheni ya Ulaya wa wasaka hifadhi na wahamiaji na kutekeleza mifano bora iliyomo kwenye ripoti hii.

Kati yam waka 2014 na 2018, zaidi ya wakimbizi na wahamiaji watoto 70,000 ambao hawakuwa wameambatana na wazazi au walitenganishwa na wazazi waliingia Italia kwa njia ya bahari ambapo walikuwa na umri wa kati ya miaka 15 na 17.

Yakadiriwa kuwa 60,000 kati yao hao wametimiza umri wamiaka 18 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.