Kwa mara ya 28 Baraza Kuu la UN lataka vikwazo dhidi ya Cuba viondolewe, Brazil yapinga

7 Novemba 2019

Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo kwa kishindo wamepitisha azimio la kuitaka Marekani iondoke vikwazo vvyka dhidi ya Cuba.

Katika kura iliyopigwa hii leo mataifa 187 yaliunga mkono azimio hilo ilhali nchi Marekani, Israel na kwa mara ya kwanza Brazil walipinga huku Ukraine haikushiriki kupiga kura.

Marekani iliiwekea Cuba vikwazo mwaka 1960 na tangu mwaka 1992, kila mwaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa likipiga kura kulaani vikwazo hivyo na kutaka viondolewe.

Kabla upigaji kura hii leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bruno Rodríguez Parrilla, alieleza wajumbe kuwa, “hivi karibuni serikali ya Rais Donald Trump ilianza kuendeleza uingiliaji wake kwa Cuba kwa kuanzisha mikakati ili kuzuia upelekaji wa mafuta nchini mwetu kwa kutumia vikwazo na vitisho kwa meli, kampuni za meli na zile za bima kutoka maeneo mbalimbali.”

Kwa mujibu wa Bwana Rodríguez Parrilla lengo la Marekani ni  kutibua uchumi wa Cuba na kuharibu hali ya maisha ya familia za wananchi wa taifa hilo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kelly Craft amesema, “kama ilivyo kwa mataifa  yote, tuna haki ya kuchagua mataifa ambayo tunafanya nayo biashara. Hii ni haki  yetu. Kwa hiyo inatia shaka kuwa jamii ya kimataifa kwa kisingizio cha kulinda mamlaka, inaendelea kuhoji haki hiiyo.”

Moja ya mitaa kwenye eneo la Camajuaní, manispaa ya mji wa Villa Clara nchini Cuba
PAHO/WHO
Moja ya mitaa kwenye eneo la Camajuaní, manispaa ya mji wa Villa Clara nchini Cuba

Balozi Craft ameendelea kusema kuwa, “kile kinachotia hofu zaidi ni kwamba kila mwaka, hiki chombo kinatetea dai ya kwamba utawala wa Cuba hauna njia nyingine zaidi ya kuonea watu wake kwa kisingizio cha vikwazo.”

Venezuela nayo haikusalia nyuma ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje Jorge Arreaza amesema kuwa ni wakati wa sauti ya walio wengi isikike, “siyo tu nchi wanachama bali pia kutoka kwa watu wa dunia ambao kwa pamoja wanadai kuondolewa mara moja na kabisa vikwazo vya kiuchumi na kibinadamu dhidi ay Cuba.”

Amesema ni wakati wa kumaliza viwango tofauti vya misimamo katika uhusiano wa kimataifa.

Hii ni mara ya 29 kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeridhia azimio la kutaka Marekani iondoe vikwazo dhidi ya Cuba.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter