Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zaidi na za pamoja zahitajika kulinda mazingira kwenye maeneo ya mizozo-UNEP

Uharibifu mkubwa nchini  Iraq uliotekelezwa na ISIL.
UNICEF/Sparks
Uharibifu mkubwa nchini Iraq uliotekelezwa na ISIL.

Juhudi zaidi na za pamoja zahitajika kulinda mazingira kwenye maeneo ya mizozo-UNEP

Amani na Usalama

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, limesema licha ya kuwepo kwa mbinu tofauti za kulinda mazingira, bado mazingira yanaendelea kuwa muathirika wa kimya wa mizozo ya vita kote ulimwenguni.

Katika ujumbe wake wa siku ya kuzuia uharibifu wa mazingira katika vita na mizozo,  Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen amesema katika miongo miwili iliyopita kumekuwa na mabadiliko mawili makubwa ambayo yameathiri uelewa wa jamii ya kimataifa kuhusu changamoto za amani na usalama.

Ametaja mabadiliko hayo kuwa ni mosi, kuongezeka kwa wigo wa wahusika katika mzozo na kujumuisha pande zisizo za kitaifa, pia, “usalama hautizamwi kama vitisho vya kijeshi. Leo hii, udhaifu wa taifa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ni moja ya tishio kubwa ya amani kimataifa.”

Pili ni kueleweka zaidi kwa vichochezi vya ukosefu wa usalama na kwamba “ ripoti ya mwaka 2004 ya jopo la ngazi ya juu la Katibu Mkuu  kuhusu vitisho, liliangazia changamoto na mabadiliko kati ya uhusiano wa mazingira, usalama, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kufikia amani kimataifa ifikapo karne ya 21”.

Bi Andersen, amesema, sababu za kimazingira sio hata ikitokea sababu ya mizozo ya kikatili. 

Hata hivyo, uharibifu wa rasilimali za asili na shinikizo kwenye mazingira katika nyanja zote za mzozo vinachangia katika kukua na kutekelezwa kwa ukatili ambao unakwamisha uwezekano wa amani.

Amesema upatikanaji wa maji, uharibifu wa ardhi, mafuriko na uchafuzi ukijumuisha na ugombeaji wa rasilimali za kuchimba vyote vinaweza kuongeza uhasama ambao unachangia katika mizozo kama ilivyo katika uharibifu wa mazingira ikiwemo, ukataji wa miti, mmomonyoko wa udongo na ongezeko la majangwa.

UNEP imeonya licha ya hatua za kulinda mazingira zilizopo, ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, dunia inahitaji kwa haraka na kwa pamoja kupunguza vitisho dhidi ya mazingira  vitokanavyo na mizozo ya kujihami ambavyo vinatishia mazingira na hatimaye afya na mbinu za kujipatia vipato.