Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taka za elektroniki zageuka mali Nigeria:UNEP 

Kifaa cha kompyuta kilichotupwa kikitambuliwa kama taka za kielektroniki. Taka hizi zina dutu ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.
ITU
Kifaa cha kompyuta kilichotupwa kikitambuliwa kama taka za kielektroniki. Taka hizi zina dutu ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.

Taka za elektroniki zageuka mali Nigeria:UNEP 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa,  UNEP, limesema taka za kielektroniki ni mbaya na hatari kwani haziyeyuki na zinachafua mazingira. Hata hivyo hivi sasa baadhi ya vijana katika nchi mbalimbali ikiwemo Nigeria wameamua kuwa wabunifu na kugeuza taka hizo kuwa mali.

Katikati ya jiji la Lagos mji mkuu wa Nigeria taka za elektoniki kwa miaka zimekuwa shida kubwa lakini sasa zageuzwa kuwa thamani kwa kutumia mchakato mbadala wa kiuchumi.

Lengo la mchakato huo ni kulinda mazingira na kutoa ajira salama kwa maelfu ya Wanigeria na hasa vijana.

Kwa mujibu wa UNEP kila mwaka Nigeria inazalisha tani 290,000 za taka za elektoniki pamoja na kupokea zaidi ya tani 70,000 za vifaa vilivyotumika kwa elektoniki kutoka katika mataifa yaliyoendelea.

Lakini sasa vifaa hivyo vya elektroniki vikifikia mwisho wa matumizi yake na kutupwa vinakusanywa na vijana kutoka sekta isiyorasmi na vifaa ambavyo bado vinaweza kutumika vinasafishwa na kuuzwa tena na visivyofaa vinaharibiwa au kuchomwa katika maeneo maalum ya kutupa taka hizo na kuwapatia kipato vijana hao.

Hata hivyo wataalam wa afya wanaonya kwamba kemikali za sumu zilizo katika taka za elektroniki zinasababisha madhara ya ngozi, matatizo ya kupumua, kupunguza maisha ya wanaoziharibu, kuchafua hewa, maji na udongo.

Katika kuepukana na yote haya UNEP inasema sasa Nigeria inaboresha sheria ya uwajibikaji kwa watengenezaji ili kuhakikisha wanawajibika na bidhaa wanazozalisha kwa muda wote wa mzunguko wa maisha ya bidhaa hizo.

Kwa mantiki hiyo sekta salama na hyenye ufanishi ya matumizi mbadala ina fursa kubwa kwa uchumi wa Nigeria, kwani vifaa hivyo vya elektoniki vilivyoharibika vina vitu vyenye thamani kubwa ndani yake kama dhahabu, madini ya platinum na vitu vingine adimu vya thamani.

Sekta hiyo ya kushughgulika na taka za elektroniki sasa inatoa ajira kwa watu zaidi ya 100,000 Nigeria.