Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 54 wasafirishwa na UNHCR toka Niger hadi Italia

Wahamiaji na wakimbizi wakisubiri kupandisha mizingo yao kwenye ndege tayari kwa kuhamishwa kutoka Tripoli Libya
IOM TRIPOLI
Wahamiaji na wakimbizi wakisubiri kupandisha mizingo yao kwenye ndege tayari kwa kuhamishwa kutoka Tripoli Libya

Wakimbizi 54 wasafirishwa na UNHCR toka Niger hadi Italia

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limewahamisha wakimbizi 54 wasiojiweza kutoka kwenye kituo cha muda cha dharura  na maeneo ya mijini ya Niger na kuwapeleka nchini Italia.

Kundi hilo la wakimbizi waliowasili leo nchini Italia linajumuisha wakimbizi kutoka Eritrea, Ethiopia, Somalia na Sudan wakiwemo watoto 23 na 13 kati ya watoto hao wametenganishwa na wazazi wao au familia zao.

Wengi wa wakimbizi hawa walikuwa wanashikiliwa nchini Libya kwa muda mrefu ambako walikabiliwa na hali mbaya , kukiukwa kwa haki zao za binadamu  na ongezeko la tishio la kujikuta wako katika ukatili wa hali ya juu.

Wakimbizi nchini Libya wanaendelea kukabiliwa na hali mbaya, wakihaha kupata fursa za mahitaji ya msingi ili kuweza kuishi” amesema Jean-Paul Cavalier mwakilishi wa UNHCR nchini Libya akiongeza kwamba “kwa kuwakaribisha nchini Niger na kuandaa kuwahamishia nchini Italia nchi zote mbili zimeonyesha mshikamano unaohitajika dhidi ya wakimbizi. Hata hivyo maelfu zaidi ya wakimbizi hao wanahitaji msaada kama huo. Ni muhimu sana kwa nchi kujitokeza na maeneo zaidi na mchakato wa haraka  ili kusaidia kuwahamisha wakimbizi wasiojiweza kutoka nchini Libya kupelekwa kwenye usalama.”

Hii ni safari ya pili ya msaada wa kibinadamu wa kuwahamisha wakimbizi kutoka nchini Niger kwenda Italia kwa kutumia ndege ya UNHCR.

Mbali ya zoezi la leo UNHCR imewahamisha zaidi ya wakimbizi  na waomba hifadhi 5,100 kutoka nchini Libya na kuwapeleka katika nchi zingine tangu mwaka 2017, wakiwemo 2913 kuwapeleka Niger na 189 kuwapeleka Rwanda hivi karibuni.